Imeelezwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imeweza kwa kiasi kikubwa kusogeza mbele maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, huduma za afya, miundombinu, maji pamoja na maendeleo ya kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo Covid 19 ambayo imesababisha kuchelewa kwa baadhi ya mipango.
Hayo yamebainishwa Julai 17 mwaka huu na Mjumbe wa Sekretarieti ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Dkt. Crispin Ryakitimbo kwenye semina elekezi ya uelimishaji umma ngazi ya Mikoa kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Crispin Ryakitimbo akitoa wasilisho kuhusu mafanikio ya Dira ya Maendeleo ya 2025 na mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo 2050.
Dkt. Crispin amesema utekelezaji wa Dira ya 2025 umechochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa zaidi ya 6% kwa mwaka tangu mwaka 2,000 na umewezesha kuongezeka kwa kipato cha mwananchi kufikia wastani wa sh. 2,844,641 mwaka 2022 kutoka sh. 1,621,445 mwaka 2013 na chini ya shilingi milioni moja mwaka 2,000.
Amesema, Dira hiyo pia imeongeza upatikanaji wa huduma za jamii zikiwemo elimu, afya, maji, uchukuzi, mawasiliano na usafirishaji hususan viwanja vya ndege na bandari na kwamba mafanikio haya yanatokana na uwepo wa dira inayoongoza katika kufanyia kazi vipaumbele vilivyopo.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akizungumza na wadau wa maendeleo wakati akifungua semina elekezi ya uelimishaji umma kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesisitiza Viongozi mbalimbali Mkoani humo walioshiriki kikao hicho kushirikisha wadaumbalimbali kwenye mchakato wa maandalizi ya Dira hiyo ili kupata maoni yatakayo isaidia nchi katika kukua zaidi kiuchumi.
Aidha, ameongeza kuwa dira ya maendeleo ya Taifa ina gusa makundi yote, hivyo anatarajia ushirikishwaji mpana wa wadau wote, ngazi zote zikiwemo taasisi za elimu, sekta binafsi, na asasi za kiraia na mwananchi mmoja mmoja.
Nae, Bi. Senerina Kateule Makamu Mkuu wa chuo cha Taasisi ya elimu ya watu wazima (WAMO)Mkoa wa Morogoro amesema kupitia semina hiyo atahakikisha kuwa anatoa elimu kwa wafanyakazi pamoja na wanafunzi wa Chuo hicho ili waweze kutoa maoni kuhusu Dira ya taifa 2050.
Aidha, Bi. Senerina ameongeza kuwa Dira ya maendeleo 2025 imeisaidia sekta ya elimu kukuwa ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vyuo vya kati ambayo itawasaidia wanafunzi kujiendeleza kielimu na kuwaondolea wazazi mzigo wa ada kwa watoto wao.
Dira ya Maendeleo 2025 ilianza kutekelezwa mwaka 2000 na utekelezaji wake utakamilika 2025 na kuaza kutekeleza Dira hiyo 2050 huku lengo likiwa ni kuiwezesha nchi kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba (katikati walio kaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa timu ya uandishi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, viongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na wadau wa Maendeleo baada ya semina elekezi ya uelimishaji umma.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.