Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishari, Mhe. Dkt. Dotto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania - TANESCO Kukarabati vituo vya Kufua umeme ili kuondoa changamoto za kukatika kwa nishati hiyo mara kwa mara.
Naibu Waziri Dotto Biteko ametoa agizo hilo Aprili Mosi 2024 akiwa Kidatu Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro alipofanya ziara ya dharura katika mitambo ya kufua umeme ya Kidatu kufuatia kufeli kwa Gridi ya Taifa.
Tatizo hilo limejitokeza jana usiku na kusababisha Mikoa mingi ya Tanzania Bara na Visiwani kukosa umeme na kusababisha adha kwa watanzania, hali iliyompelekea kiongozi huyo kuwaomba radhi watanzania kufuatia hitilafu hiyo.
“Nawaomba radhi sana wananchi na watanzania kwa ujumla kufuatia hitilafu hiyo kwenye mfumo wa Gridi” amesema Mhe. Dotto Biteko
Hata hivyo amewaagiza viongozi wa TANESCO kuhakikisha wanatafuta suluhu ya kudumu ya kufeli mara kwa mara kwa mfumo wa Gridi hiyo ya Taifa kwa kufanya upembuzi wa kina ili kuboresha miundombinu kwenye Gridi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyoba ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima katika ziara hiyo ya Naibu Waziri Mkuu, amewashukuru viongozi wa Wizara ya Nishati kwa kuchukua hatua ya mapema ya tatizo hilo na kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umemem Tanzania – TANESCO Mhe. Gissima Nyambo – Hanga ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi watanzania kwa kukosekana kwa huduma ya umeme kufuatia hitilafu hiyo kwenye Gridi ya Taifa.
Aidha, amempongeza Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dotto Bitteko kwa kulichukulia uzito tatizo hilo na kuacha shughuli zake, kuungana na wataalamu wa TANESCO ili watanzania wapate umeme na akawahakikishia watanzania kuwa umeme umekwisha rejea kwa mikoa iliyokuwa imekosa nishati hiyo.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.