Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Seleman Jafo (mb) amemusgiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kuunda timu ya watu nane (8) wakishirikiana na Mkoa, Msajili wa Hazina (TR) ili kuangalia viwanda ambavyo havifanyi vizuri katika Mkoa wa Morogoro na kuona jinsi gani viwanda hivyo vinaenda kufufuliwa na kuanza uzalishaji kama vingine kikiwrmo Kiwanda cha Mkwawa Tobacco Leaf Co Ltd .
Mhe. Dkt. Jafo ametoa agizo hilo leo Julai 20, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Mkoani Morogoro ambapo alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha Alliance one, Mkwawa Tobacco Leaf Co Ltd, Mazava Fabrics and production East Africa Ltd na kiwanda cha kuchakata mchele cha MW Rice Mills Ltd (KORIE).
Dkt. Jafo amesema kama Wizara ya Viwanda na Biashara wanampango wa kuurudisha Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa viwanda kama ilivyokuwa mwazo ili kuwezesha vijana kupata ajira katika viwanda hivyo na kuongeza mapato katika mkoa huo, kuajiri vijana na kuinus uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.
".. Naomba nimuagize Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara aunde timu ya watu takribani 8 itakayohusisha Mkoa na Msajili wa Hazina (TR) kwenda kuangalia viwanda ambavyo havifanyi vizuri kuhakikisha vinaiga kiwanda cha Mkwawa Tobacco Leaf Co Ltd kinavyofanya vizuri..." Amesisitiza Dkt. Jafo.
Aidha Dkt . Jafo ameupongeza uongozi wa kiwanda cha Mkwawa Tobacco Leaf Co Ltd kwa uwekezaji mkubwa ambapo amehimiza kiwe cha mfano wa kuigwa kwa viwanda vingine, huku kiwanda hicho kikizalisha ajira za moja kwa moja 600 na ajira za msimu zaidi ya 3000 ambapo ajira hizo zimepunguza ongezeko la vijana kutokuwa na ajira mtaani.
Aidha, Pia Waziri huyo ameitaka mikoa mingine hapa Nchini kuhakikisha viwanda ambavyo vimekaa muda mrefu bila kufanya vizuri, vinasimamiwa na kuratibiwa ili kuhakikisha vinaanza uzalishaji wa bidhaa ambazo zitaenda kushindana katika soko la kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru waziri Jafo kwa kufanya ziara Mkoani humo na kwamba ziara hiyo itaenda kutatua changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya viwanda na biashara.
Sambamba na hilo amemshuruku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka jitihada mbalimbali katika kuhakikisha viwanda Mkoani Morogoro vilivyoacha uzalishaji vinarejea kuzalisha na kuweza kuzalisha ajira kwa vijana.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanya biashara Mkoani Morogoro Bw. Mwadhini Mnyanza amesema Mkoa wa Morogoro unajumla ya viwanda 12 ambapo viwanda saba kati ya hivyo havifanyi kazi na viwanda vitano vinafanya kazi ambapo suala hilo Waziri mwenye dhaman amelichukua na kwenda kulifanyia kazi kwa sababu ya umuhimu wake hasa katika suala la ajira kwa vijana na kuongeza mapato Serikalini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.