Waziri wa viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ametoa salamu za pole kwa ndugu jamaa, marafiki na watanzania wote kwa msiba mzito wa watu 11 waliopoteza Maisha na wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika kiwanda cha Sukari cha Mtibwa cha Mkoani Morogoro baada ya kutokea hitilafu kiwandani hapo.
Dkt. Kijaji ametoa salamu hizo za pole leo Mei 23, 2024 mara baada ya kuwasili kiwandani hapo na kukagua eneo la tukio na kisha akazungumza na vyombo vya Habari kuhusu vifo vya ndugu hao 11 waliopoteza Maisha baada ya kuunguzwa na joto la mvuke baada ya bomba la kusafirishia mvuke huo (Boiler) kupasuka.
Akiwasilisha salamu hizo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kijaji amesema Mhe. Rais anawapa pole sana na anawataka kuwa na subri katika kipindi hiki kigumu na kwamba huo ni msiba wa taifa.
“……Mheshimiwa Rais anawapeni pole sana sana kwa ajali hii na anawaomba moyo wa Subira mnapopita katika kipindi hiki kigumu…huu ni msiba wa taifa tumetikisika kama taifa kwa ajali hii tulioipata…” amesema Dkt. Kijaji
Amesema watu 11 waliopoteza maisha watatu ni raia wa kigeni, na kwamba ajali hiyo imetokea wakati wanakamilisha azma ya Serikali ya Tanzania ya kuondoa changamoto ya upungufu wa sukari hapa nchini kuanzia mwaka 2025 kwa kwa makubaliano ya viwanda vyote vya sukari kuzalisha zaidi ambapo mpango huo kwa upande wa kiwanda cha mtibwa ulipangwa kuanza leo Mei 23,2024.
Akitoa salamu za pole ngazi ya Mkoa kwa wafiwa na jamii yote ya Kiwanda cha Mtibwa Mkuu wa MKoa wa Morogoro Mhe. Adam Ali Kighoma Malima amesema gharama za kusafirisha miili ya marehem hao zitagharimiwa na Kiwanda hadi watakapowasitiri.
Aidha, Mhe. Adam Malima amebainisha kuwa kiwanda hakitafanya kazi ndani ya kiwanda hicho kwa siku tatu kwa ajili ya maombolezo na kufanya uchunguzi wa miundombinu ya eneo lililotokea ajali endapo liko salama ili baada ya siku tatu kazi ziweze kuendelea.
Awali kiongea na vyombo vya Habari kuthibitisha ajali hiyo, Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Shaban Marugujo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku Mwenyekiti wa makampuni ya super Group Seif A. Seif amewashukuru wananchi wote kwa kuonesha utulivu na mshikamano kwa kipindi chote maombolezo kwenye msiba huo mkubwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.