Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amekabidhi kompyuta 11 pamoja na Vichapishi (printer) kwa Halmashauri 7 za Mkoa huo zikiwa na lengo la kukusanya, kuhifadhi taarifa na kuboresha huduma za UKIMWI katika vituo vya Matunzo na Tiba ya UKIMWI kwenye Halmashauri hizo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi kompyuta hizo leo Februari 15 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Mussa amesema, kompyuta hizo zimenunuliwa na fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa zilifanyika Mkoani Morogoro Disemba Mosi, 2023.
Amebainisha kuwa jumla ya fedha zilizokusanywa kwenye maandalizi ya sherehe hizo ni Tsh. 50,000,000/= na baada ya matumizi kwenye sherehe hizo, fedha zilizobaki zimeelekezwa kununua vifaa hivyo ambavyo ni Kompyuta na vichapishi kwa lengo lilelile la kuboresha huduma za masuala ya UKIMWI.
Katika hatua nyingine Dkt. Mussa amewataka Waratibu wa UKIMWI wa Halmashauri saba zilizokabidhiwa kompyuta hizo kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhamasisha wadau kuendelea kuwa na moyo wa kuchangia.
“...lakini mkazitunze sasa ili zitumike kwa muda mrefu na kuleta manufaa yale yanayotakiwa...” amesema Dkt. Mussa.
Naye Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (RASHCo) Mkoa wa Morogoro Dkt. Neema Mtambo amesema kompyuta hizo zitagawanywa katika vituo 11 vya Matunzo na Tiba ya UKIMWI kwenye Halmashauri saba, lengo likiwa ni kuboresha huduma na takwimu za UKIMWI.
Aidha, Dkt. Neema ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kuboresha Sekta Afya huku akiwashukuru wadau waliochangia fedha hizo na kuahidi kuwa atasimamia ili kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini kutoka Halmashauri ya Mvomero Dkt. Grace Emil kwa niaba ya Waratibu wa UKIMWI wa Wilaya amesema vifaa hivyo vitasaidia wananchi kutosafiri umbali mrefu kufuata huduma za UKIMWI na kupata takwimu sahihi na kurahisisha kazi katika Halmashauri hizo.
Halmashauri zilizopata kompyuta na Vichapishi hivyo ni Pamoja na Halmashauri ya Malinyi, Mlimba, Morogoro DC, Ulanga, Mvomero, Gairo na halmashauri ya Kilosa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.