Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali mussa amewaagiza Watendaji wa Kata kuhakikisha katika Kata zao kunakuwa na Baraza la Usalama la Kata ambalo litaenda kusaidia katika kujadili changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kuweza kuzitatua kwa wakati.
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na watendaji wa kata wote wa Mkoa wa Morogoro yaliyofanyika katika ukumbi wa mbaraka mwinshehe uliyopo halmashauri ya manispaa ya Morogoro.
Dkt. Mussa amesema Baraza hilo litaundwa na Mtendaji wa Kata, Polisi Kata pia Wenyeviti wa vijiji ambapo amesema baraza hilo litasaidia kuwakutanisha na kufanya vikao ili kuibua na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika kata husika.
"..Tulipanga na kuelekeza kwamba katika kila Kata ni lazima kuwepo na kitu kinachoitwa Kamati ya Usalama ya Kata.." Amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amewataka watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wote wa Mkoa huo kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano na kila mmoja atekeleze wajibu wake ili kuweza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo wanayosimamia kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla kwa sababu wao ni injini ya maehdeleomhayo.
Aidha, Kiongozi huyo amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji wa kata kutokaa katika vituo vyao vya kazi ama kukaa mbali na vituo vyao huku akibainisha kuwa hali hiyo inatokana na Maafisa Tarafa kutowasimamia ipasavyo Watendaji hao hali inayosababisha uwepo wa utendaji mbovu wa kazi.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo amekemea baadhi ya viongozi hao wa Serikali kujihusisha na kupokea rushwa na wengine kuwana tabia za ulevi kitu ambacho kinasababisha kutowajibika katika kazi hivyo amesema hatua kali zitachukuliwa kwa mtendaji yoyote atakaye kwenda kinyume na maadili hayo ya Serikali.
Kwa wao Maafisa Tarafa kupitia Afisa Tarafa wa Mgeta Bw. Fabius Byamungu wamesema wamejifunza vema masuala ya utawala bora, utunzaji fedha na kuandaa bajeti pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na kwamba amafunzo hayo yataleta chachu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, hivyo wameishukuru OR- TAMISEMI kwa kuleta mafunzo hayo.
Naye Afisa Mtendaji Kata ya Mafiga Bi. Amina Saidi amesema mafunzo hayo yataenda kuwasaidia katika kutekeleza kazi kulingana na vyeo vyao kama watendaji wa kata, pia yatasaidia katika uwasilishaji wa taarifa ngazi kwa ngazi na kubadili kabisa utendaji wao wa kazi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.