Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkat. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya ile inayotumika sasa kuonekana inazidiwa katika utoaji wa huduma ya Afya kwa wagonjwa.
Dkt. Samia Suluhu Hassan amebainisha hayo wakati akiongea na wananchi wa Mkoa huo leo Agosti 6, 2024 katika uwanja wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Rais Samia amemuagiza waziri mwenye dhamana hiyo Mhe. Ummy Mwalimu na kumtaka atoe shilingi bilioni 5 za kuanzia ili ujenzi huo uanze mara moja hata kama kwa awamu tofauti.
".. Nilikuwa na Waziri wa Afya nikampa maelekezo aende akapekue kwenye vifungu vyake angalau apate bilioni 5 za kuanzia na tuanze ujenzi wa hospitali hiyo ya rufaa,
.." amesisitiza Dkt. Samia.
Amesema, fedha hizo shilingi bilioni 5 zianze kujenga majengo ya kutolea huduma ya mama na mtoto na fedha nyingine zitakaletwa baadae zitaendeleze pale walipoishia.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo baada ya maombi ya mbunge wa Morogoro mjini Abdul aziz Mohamed Abood kutoa ombi hilo la kupata hospitali ya rufaa ambalo ni ombi la siku nyingi baada ya kuona hospitali inayotumika sasa kuonekana inazidiwa na wingi wa wagonjwa
Akizungumzia juu ya Morogoro ya viwanda, Dkt. Samia amesema Serikali ya awqmumya sita imedhamiria kurudisha hadhi ya Morogoro, kuwa Mkoa wa viwanda huku akitaja kufufuliwa kwa kiwanda cha kuchonga vipuli cha mang'ula kilichpo Wilayani Kilombero mkoani humo.
Hata hvyo amesema lengo la kurejesha mkoa huo kuwa Mkoa wa viwanda ni kutaka kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana Mkoani humo na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu utunzaji wa mazingira Rais Dkt. Samia Suluhu amesema pamoja na umuhimu wa mabonde ya hapa nchini, bonde la Kilombero lina umuhimu zaidi kutokana na bonde hilo kuwa ni moja ya chanzo kikuu cha mradi mkubwa wa kufua umeme katika bwawa la Mwalimu Nyerere.
Hivyo ametoa wito kwa wanamorogoro kulitunza bonde hilo lenye hekta 55 kwa kutoa ushirikiano pale Serikali itakapoanza kutekeleza azma yake ya kulijenga kwa lengo la kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuzuia mafuriko ambayo kutokea karibu kila mwaka hivyo bonde hilo liweze kuleta raha kwa wananchi badala ya karaha.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amezungumzia Mkoa wa Morogoro kuwa ni Mkoa wa uzalishaji wa mazao ya chakula na kwamba unategemewa na Taifa hususan katika zao la mpunga ambalo linazalishwa kwa wingi kuliko mikoa yote hapa nchini.
Pia amebainisha kuwa Mkoa wa Morogoro una kiwanda cha kuchakata mchele na mmiliki wake ndiye mnunuzi mkubwa wa mchele hapa nchini ambapo ananunua shilingi 900 kwa kila kilo moja.
Kabla ya kufanya mkutano na wananchi wa Morogoro, Dkt. Samia Suluhu Hassan alianza ziara ya leo kwa kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza sigara cha Serengeti Cigaratte Company Limited na kisha kuzindua majengo ya maabara jumuishi ya Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Kesho Agosti 7, 2024 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anategemea kukamilisha ziara yake ya siku sita (6) Mkoani Morogoro kwa Kuzindua kiwanda cha Sukari cha mkulazi kilichopo Kilosa Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.