Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka mamlaka za Mikoa na Wilaya hapa nchini kuhakikisha wanawasimamia vyema wenyeviti wa vijiji na watendaji wengine wa Serikali ngazi hiyo katika kutekeleza kazi zao kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni kwa lengo la kuepusha migogoro ya ardhi.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo Agosti 3, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya TUTUNZANE Wilayani Mvomero inayolenga kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Aidha, amewataka viongozi hao kutumia kampeni mbalimbali zakuleta suluhisho kwa njia ya Amani badala ya kutoa matamko.
Amebainisha kuwa kilio kilichopo ni kwamba baadhi ya viongozi hao wa ngazi ya vijiji hawasimamii ipasavyo serikali za vijiji, badala yake wanasubiri wananchi wakishaumizana uko ni rahisi kunyoosha mkono kupokea kuliko kuleta suluhu.
Aliwataka kuwasimamia wenyeviti wa vijiji waache kunyoosha mikono ,na walete suluhu za kweli na sheria lazima zifuatwe.
Rais Samia pia amemtaka kila Mwananchi kuheshimu Uhuru wa mwenzake kwa kila shughuli anayoifanya ikiwemo ya kilimo na ufugaji kwani wote wanategemeana katika maisha ya kila siku.
Amewataka wakuu wa wilaya na mikoa kuwachukulia hatua wale wote watakaoingilia uhuru wa wenzao kwa manufaa binafsi.
" Kila mmoja aheshimu mipaka ya mwenzie, kama unataka kulisha mifugo kalishe kwenye malisho sio kwenye mashamba, nanyie wakulima acheni kukata mifugo ya wenzenu" alisema.
Rais ameonesha kuridhishwa na kampeni hiyo ya kimkakati ya TUTUNZANE MVOMERO na amesema Serikali itausimamia vema huku akiutaka uongozi wa Mkoa na wilaya ya Mvomero pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuusimamia mradi huo wa mfano kwa kutenga bajeti na kuwashirikisha wananchi kikamilifu.
Rais alitumia fursa ya mkutano huo kuwapatanisha wakulima na wafugaji kwa kuwataka wapeane mikono kama ishara ya kumaliza migogoro yao.
"Maugomvi mwisho leo na kwamba sasa wote mnakwenda kubadilika na kuingia kwenye mradi mkabadilike mlime mnaolimanna mnaofuga mkafuge, hakuna haja ya kugombana, mtumie mradi huu ,nyie wote mnatupa uhai na mnatupa vitoweo na vyakula" amesema.
Awali akizindua bwawa la umwagiliaji la Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza mawaziri wenye dhamana kuwa katika masuala yote ya ujenzi wa mabwawa, Maafisa Mazingira ngazi ya Taifa washirikishwe kikamilifu na kwamba suala la mazingira litiliwe maanani. .
" Hapa niweke msisitizo, nimeona kazi nzuri mnayofanya ya ujenzi wa mabwawa, tumieni maafisa Mazingira, suala la Mazingira litiliwe maanani, kwenye mabwawa, kiwandani na mashambani" alisema..
Aidha Rais Samia alisema Serikali itaendelea kulinda makundi yote na inapotokea imeegemea upande mmoja wa wanyonge hivyo upande mwingine usione vibaya kwani serikali inasimamia na kutetea maslai ya makundi yote.
" ikitokea sukari imepanda hadi shilingi elfu saba lazima serikali isimame na wananchi kwani ndio walaji na chakula ndio kila kitu " alisema.
Alipongeza uongozi wa kiwanda cha Mtibwa kwa kutoa ajira zaidi ya 8000 kwa vijana na ajira 9000 kwa wakulima wa nje ambapo upanuzi ukikamilika zitafikia ajira ya watu 11,000
Hata hivyo Raisa Samia amesema Serikali katika kuthamini wawekezaji imeondoa msamaha wa kodi shilingi bilioni 246 kwa viwanda 5 ambapo kwa kiwanda cha Mtibwa pekee msamaha wa kodi ni shilingi bilioni 80.9 .
"Nimeambiwa uwekezaji wa kiwanda cha Mtibwa ni Dola milioni 155 na kwamba upanuzi wake ukikamilika utafikia dola milioni 805, huu sio uwekezaji mdogo, tulizoea kuona uwekezaji kama huu kwa wawekezaji wa nje lakini leo yupo huyu wa ndani " alisema.
Awali mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi kiwanda cha Sukari cha Mtibwa Seif Ally Seif alisema wa kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto ya umeme ambapo kati ya pampu 6 zinazopampu maji katika bwawa hilo ni mbili tu zinafanya kazi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.