Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imezindua huduma ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika shule ya sekondari ya Morogoro na kituo cha kulelea wazee cha Fungafunga katika Manispaa ya Morogoro ili kuunga mkono ajenda ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya kutunza mazingira kwa kutumia nishati safi zikiwemo gesi asilia, umeme na Mkaa mweupe hivyo kulinda afya za watanzania na kulinda mazingira.
Mradi huo umezinduliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko mara baada ya kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa EWURA kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Nashera mkoani Morogoro kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya Mamlaka hiyo.
Akifafanua zaidi, Naibu Katibu Mkuu amewapongeza EWURA kwa kuwa mfano kwa kutenga Tsh. Mil 40 kwa ajili ya ununuzi majiko ya kisasa 6 na mtungi wa gesi wa lita 1000 na katika kituo cha kulelea wazee cha Fungafunga kutoa majiko 3 na mitungi 3 kwani kutasaidia wanafunzi zaidi ya 700 wa shule ya Sekondari hiyo na wazee wasiopungua 104 wa kituo cha Fungafunga kupunguza matumizi ya kuni, muda na idadi ya magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni.
“… niwashukuru EWURA kwa kutoa msaada wa Tsh. Mil. 40 kwa kwani umewezesha wanafunzi wa shule hii kupata majiko 6 ya gesi na mtungi wa lita 1000…” amesema Naibu Katibu huyo
Katika hatua nyingine, Dkt. James amewataka EWURA kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Nishati na Maji hususan petroli, gesi asilia na maji na kuendelea kutoa huduma kwa uwazi, ubunifu, ufanisi na weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Mwainyekule amesema taasisi hiyo imechukua hatua za mapema kuisadia jamii kwani mpango mkakati wa serikali ni kuhakikisha kila sehemu yenye watu zaidi ya 100 wanatumia nishati safi ya kupikia hivyo Baraza la Wafanyakazi wa EWURA limetoa zaidi ya Tsh. Mil 40 kwa ajili ya ununuzi wa majiko, mitungi pamoja na kuhakikisha ukamilishaji wa huduma hiyo katika shule ya Morogoro na kituo cha wazee cha Fungafunga.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha ametoa shukrani za dhati kwa EWURA kwa kukamilisha huduma hiyo kwani amesema kutachochea mashirika na taasisi nyingine kutoa misaada kwa wingi na kuahidi kushirikiana na walimu ili kuitunza miundombinu iliyotolewa.
Kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, Bi. Kundi Aloyce mwanafunzi wa kidato cha sita ameishukuru Serikali pamoja na EWURA kwa kuwajengea miundombinu ya kutoa huduma ya nishati safi ya kupikia yakiwemo majiko ya kutumia gesi kwani amesema hapo mwanzo kuni ziliwacheleweshea muda na kula chakula chenye kunukia moshi.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mpango mkakati kuwa ifikapo 2034 matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia yafikie 80% ya watanzania wanaotumia nishati hizo hapa nchini.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.