Wajumbe wa mkutano wa Wadau wa masoko ya mazao ya kilimo na mfumo wa stakabadhi ghalani katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo wameupokea kwa mikono miwili uuzaji mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani huku lengo likiwa ni kuinua kipato cha wakulima wenyewe pamoja na Halmashauri hiyo.
Hayo yamebainishwa Februari 8, 2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Rahel Nyangasi wakati wa Mkutano wa Wadau wa masoko ya mazao ya kilimo na mfumo wa stakabadhi ghalani Wilayani Gairo uliolenga kupeana uelewa wa pamoja kuhusu umuhim wa mfumo huo.
Mhe. Nyangasi amesema mfumo huo utaisaidia halmashauri ya Gairo kukusanya mapato mazuri ambapo kabla wanufaika walikuwa ni walanguzi hivyo ameahidi kupitisha azimio hilo kwenye kikao cha baraza la madiwani ili kuupa nguvu mfumo huo, huku akiwataka Madiwani wenzake kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu mfumo huo.
“...lakini tunaona kabisa kuwa mfumo huu sisi Halmashauri tutakusanya mapato pamoja na kupunguza matumizi...Mkurugenzi hebu andaeni paper hii kesho bahati nzuri tunalo baraza la Madiwani tuipitishe ili mpango kazi huu uanze kazi mara moja..." amesema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Aidha, ameongeza kuwa baraza la Madiwani limeupokea mfumo huo huku akimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kubuni vyanzo vya mapato ili kuitoa Halmashauri mahali ilipo sasa.
Awali, akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amesema lengo la kikao hicho ni kuwaleta pamoja wataalamu wa masuala ya Stakabadhi ghalani na kutaka Watendaji wa Halmashauri hiyo kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mfumo huo ili wakulima na Halmashauri hiyo kupata mapato hivyo kukuza uchumi wao na taifa lao.
Ameongeza kuwa, mfumo wa Stakabadhi ghalani utawasaidia wakulima kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi, hivyo amewataka wajumbe wa mkutano huo kuhamasisha wananchi juu ya umuhim wa mfumo huo katika shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Bw. David Sukali amesema Mkoa wa Morogoro kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani umewaingizia wakulima zaidi ya shilingi 12 bilioni kwa mazao ya mbaazi, ufuta na kakao huku akibainisha kuwa mfumo utawasaidia wakulima kuwa na sauti moja ya kuamua nani wamuuzie na kwa bei gani, lakini pia kuwa na uhakika wa soko kwa mazao yao.
Nao baadhi ya wakulima Wilayani humo akiwemo Mhe. Butindi Masatu ambaye ni Diwani Kata ya Kibedya ameipongeza Serikali kwa kuja na mfumo huo ambao ni suluhisho kwa wakulima na kuwaomba wadau kuyapa kipaumbele mazao yanayolimwa kwa wingi katika Wilaya hiyo yakiwemo mazao ya Ufuta, mbaazi na maharage.
Wajumbe wa kikao hicho waliazimia kuyaingiza mazao manne ya Ufuta, Korosho, Mbaazi na Maharage kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili wakulima waanze kufaidika kupitia mazao hayo.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.