Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa ameagiza Wakala wa Baraba za Mijini na Vijini (TARURA) kutomlipa mkandarasi anayejenga barabara ya Kijiji cha Lulongwe, Kata ya Matuli Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kutokana na barabara hiyo kutojengwa kwa kiwango kinachostahili.
Fatma Mwassa ametoa agizo hilo Oktoba 21, mwaka huu wakati wa ziara fupi aliyoifanya katika kata hiyo ya Matuli kwa lengo la kukagua na kujionea ujenzi wa barabara hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya ujenzi wa barabara hiyo usioridhisha.
Amesema, hajaridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo kutokana na kuwepo wa dosari nyingi katika ujenzi huo, hivyo TARURA na wataalamu wote wa barabara Mkoani humo wakae kikao cha pamoja kujadili dosari hizo na mkandarasi asilipwe hadi pale atakaporekebisha dosari hizo.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama kikagua karavati ltakalo tumika katika ujenzi wa daraja katika kijiji cha Lulongwe.
“...kwa hiyo zote hizo dosari zitarekebishwa kwanza ndipo mkandarasi awezekuchukua pesa yake, hakuna mkandarasi hata mmoja atakayelipwa bila kuwa hizi barabara zimetengenezwa vizuri kwa kiwango kinachokubalika kitaalam...” amesema Fatma Mwassa.
Sambamba na hilo Fatma Mwassa ametoa miezi miwili kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhakikisha Zahanati ya Lulongwe inapatiwa vifaa tiba kwa kuwa ujenzi wa zahanati hiyo umekamilika huku akimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kusimamia agizo hilo.
Kwa upande wao wakazi wa Kijiji cha Lulongwe akiwemo Bw. Rosta Salumu wameishukuru Serikali kutatua changamoto za wananchi kwa wakati wakiwemo wa kijiji hicho, hata hivyo wamemueleza Mkuu wa Mkoa tatizo la kijiji chao la kutoitisha mikutano ya hadhara kama inavyotakiwa, hivyo hawajawahi pia kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Nae Diwani wa Kata ya Matuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mhe. Lucas Lemomo amekiri kutokuwepo kwa mikutano ya hadhara katika Kijiji hicho na kuhaidi kuifanyia kazi changamoto hiyo.
Mkuu wa Mkoa Fatma Mwassa alifanya ziara fupi katika Halmashauri hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo usioridhisha hususan katika kijiji cha Lulongwe ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kijiji hicho na ujenzi wa Zahanati ambapo pia alikutana wananchi na kujibu baadhi ya kero zinazowakabili.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.