Katika kikao cha kutathmini utekelezaji wa mkataba wa lishe kilichofanyika Agosti 5 2022, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wakati huo Mhe. Fatma Mwassa amezisisitiza Halmashauri za Mkoa huo kuwa ndiyo kitovu cha utekelezaji wa afua za lishe kwa jamii.
Wakati akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho Mhe. Fatma Mwassa amesema Halmashauri zinatakiwa kutoa mchango mkubwa kwa wananchi wa maeneo yao ikiwemo elimu kuhusu suala zima la lishe, fedha na ufuatiliaji wa jamii.
“...Halmashauri ndiyo kitovu cha utekelezaji wa afua za lishe katika Mkoa wa Morogoro...” alisema Mhe. Fatma Mwassa.
Aidha, katika kikao hicho ameelekeza halmashauri zote mkoa Morogoro kutenga shilingi 1000 kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha lishe kwa watoto waliochini ya miaka mitano na kuzitumia fedha hizo kwa madhumuni ya kuboresha lishe kwa watoto wetu.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka akinamama kuwanyonyesha maziwa yao watoto wao kwa kipindi cha miezi sita bila kuwapa chakula kingine kwani maziwa hayo kwa mujibu wa wataalamu yanavirutubisho muhimu katika ukuaji na afya ya mtoto.
Kwa upande wake Afisa lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amesema Mkoa umejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa changamoto ya udumavu na utapiamlo zinapungua kwa kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya lishe na utoaji wa elimu ya lishe kwa jamii nzima.
Nae, Afisa lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bw. Samuel Mwita amesema ushirikiano baina ya viongozi wa dini na Serikali, wataalam wa afya, pamoja na wananchi ndiyo silaha pekee ya kuondoa kabisa ama kupunguza tatizo la lishe Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.