Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro imetenga zaidi ya shilingi Milioni 400 kutoka Katika Mapato yake ya ndani kujenga kituo Cha Afya Cha Kata ya Mbasa kwa lengo la kunusuru maisha ya mama na mtoto pamoja na kutoa huduma nyingine za Afya kwa wananchi zaidi ya 6,000 wa kata hiyo.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, alipofanya ziara Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kukagua ujenzi wa kituo cha Afya kinachojengwa katika Kata ya Mbasa.
Kituo hicho ambacho hadi sasa kimefikia asilimia 94, ujenzi wake umetanguliwa na jengo la Mama na Mtoto kwa lengo la kunusuru maisha ya kundi hilo la mama na mtoto kwa kutumia fedha zake zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo ya Mji wa Ifakara.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akiongea wakati akikagua jengo hilo la mama na mtoto Mara baada ya kukamilisha ziara yake Katika Halmashauri ya Mlimba, amewahakikishia wananchi wa Kata ya Mbasa kuwa Serikali italeta madawa, vifaa tiba na wahudumu ili wananchi wa kata hiyo na kata jirani waweze kupata huduma waliyoitarajia.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ifakara na Wataalamu wake wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godi godi kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuzitaka Halmashauri zote hapa nchini kila moja kujenga Kituo kimoja cha Afya kupitia mapato yake ya ndani.
“Huduma hii ya Afya ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali hii ya awamu ya sita, niwahakikishie wananchi wa Ifakara kwamba Serikali italeta madaktari wa kutosha ili kutoa huduma katika kituo hiki cha Afya”amesema Martine Shigela
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha wazo la kila Halmashauri kujenga jengo kuanzia msingi hadi kulikamilisha ili mapato ya ndani yaweze kuonekana kwa urahisi kwa wananchi.
“ujenzi umeshakamilika kwa asilimia 90, tunategemea hivi karibuni baadhi ya majengo yataanza kutumika” amesema Godigodi.
Naye Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Khadija Rashid Kilama ameishukuru Serikali kwa kufanikishia ujenzi wa kituo cha Afya cha Mbasa ambapo hapo awali katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kulikuwa na vituo vya Afya viwili kikiwemo cha Serikali kimoja na cha binafsi kimoja hali yoilipelekea wananchi wa hali ya chini kushindwa kupata huduma ya Afya kutokana na galama kubwa.
Diwani wa Kata ya Mbasa, Mhe. Khadija Kilama.
Sambamba na hayo amesema kujengwa kwa kituo hicho cha Afya kitakipunguzia mzigo kituo cha Afya cha Kibaoni na hivyo kumfanya Mwananchi wa chini kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu na haraka zaidi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.