Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kutekeleza azima ya mapinduzi ya kilimo kwa kulima mazao Matano ya kimkakati ya Mkoa huo ikiwemo zao la Kokoa ili kuongeza Uchumi wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Januari 10 mwaka huu wakati akikagua ghala la kuhifadhia mazao ya viungo kama karafuu lililopo Kata ya Tawa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema hayo baada ya Mkoa huo kukubaliana kulima mazao Matano ya kimkakati ambayo ni Michikichi, Kokoa, Karafuu, Parachichi na Kahawa kwa lengo la kufanya mapinduzi ya Kilimo Mkoani humo.
Kwa sababu hiyo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro pamoja na kuanza kulima mazao ya Karafuu na Michikichi ameagiza kulitizama pia zao la Kakao kwa kuwa hali ya hewa ya Halmashauri hiyo inafanana kabisa na hali ya hewa ya Tuliani Wilayani Mvomero ambayo inastawisha zao la kakao kwa wingi Mkoani humo.
“...huko juu jambo lingine kubwa, naomba tujipange kwa zao jipya la kokoa pale sijaliona, tujipange kwa zao jipya la kahawa...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na maagizo hayo, Mhe. Adam Malima ametaka ghala la kuhifadhia mazao ya viungo la Tawa kulifanya kuwa kituo cha Biashara badala ya kulifanya ghala hilo kuwa eneo la kuhifadhia mazao mbalimbali pekee.
Katika hatua nyingine wakati wa ziara hiyo alitembelea miradi ya maendeleo ambapo alitembelea ujenzi wa wa madarasa na mabweni ya wasichana ya shule ya Sekondari ya Matombo ambapo aliagiza mabweni hayo kujengewa uzio pamoja na kufanyia ukarabati madarasa chakavu ndani ya shule hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.