Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro wametakiwa kujijengea tabia ya kuwashirikisha wananchi wa eneo husika fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanyika katika maeneo yao ili kuwa na uelewa na miradi hiyo, kuanza na kukamilika kwaake.
Agizo hilo limetplewa Agosti 5 mwaka huu na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika mradi wa Zahanati ya Minepa inayojengwa baada ya Serikali kutoa pesa na wananchi kuchangia nguvu zao.
Aidha, Lt. Mwambashi amesema, wananchi wanastahili kufahamishwa kila hatua ya maendeleo ya miradi inayofanyika katika maeneo yao kwa sababu wao ndio walengwa katika ujenzi wa miradi hiyo.
Amesema fedha za miradi hiyo inayotolewa kwa ajili ya miradi kama hiyo ziwe zinakwenda moja kwa moja kwenye akauti ya kijiji husika badala ya kwenda Halmashauri ya Wilaya kwa kuwa fedha hizo zinakuwa za wananchi hao hivyo waachiwe kufanya kazi za utekelezaji wa miradi hiyo mwenyewe.
‘’Tumepita katika miradi mingi ambayo wananchi wakipewa ile pesa watendaji katika vijiji wanasimamia vizuri kwa sababu wanajua umuhimu wa vituo vya Afya na zahanati kwa wananchi, nasisitiza kwamba pesa zikija msiig’ang’anie Halmashauri waachieni wananchi wajisimamie’’ amesema Lt. Mwambashi.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la zahanati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya amempongeza kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kwa kuweka jiwe la msingi na kumuahidi kusimamia maelekezo yote aliyoyatoa.
Ngolo Malenya amesema kwa kipindi kirefu wananchi wa Kijiji cha Minepa wamekuwa wakipata changamoto ya kupata huduma ya Afya huku wakilazimika kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho akiwemo Bi. Joyce Samwel wameonekana kufurahishwa na ujenzi wa zahanati hiyo na kubainisha kuwa hiyo itakuwa suluhu ya changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nayo hususan kwa mama wajawazito.
Naye, James Mussa mkazi wa kijiji hicho, ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha za zahanati hiyo ili kupata huduma ya Afya karibu kwani amesema wananchi hususan akinamama wajawazito wameteseka kwa muda mrefu kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya hata wakati mwingine kusababisha akinamama hao kujifungua njiani.
‘’Mama wajawazito wanasumbuka sana wanapokaribia kujifungua kwa sababu hospitali ya kivukoni ipo mbali sana kiasi kwamba mama wajawazito hujifungulia njia kutokana na umbali, naamini kituo hiki sasa kitatusaidia ’’ amesema Mussa.
Mwenge wa Uhuru 2021 umekamilisha kupitia jumla ya miradi sita ya maendeleo Wilayani Ulanga Mkoani humo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bil. 8.5 bila kuwepo kikwazo chochote.
Mwenge wa uhuru wa mwaka 2021 wenye Kauli Mbiu: “TEHAMA ni Msigi wa Taifa Endelevu Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji” uanendelea kukimbizwa Mkoani Morogoro ikiwa ni siku ya tatu tangu kuingia Mkoani humo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.