Wadau wa sekta ya michezo Mkoani Morogoro wameshauri Halmashauri za Wilaya/Manipsaa na Majiji hapa nchini kutenga bajeti ili kushiriki vyema mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) pia kutoa washiriki wa mashindano hayo.
Ushauri huo umetolewa Oktoba 28 mwaka huu na Bw. Omari Kibukila ambaye ni Katibu wa chama cha Riadha Mkoa wa Morogoro na Mwenyekiti wa Kamati ya Riadha ya mashindano yanayoendelea baada ya kufanya mahojiano nae katika uwanja wa Jamhuri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Bw. Kibukila amesema kuna Halmashauri 185 hapa nchini, hata hivyo ni Halmashauri 144 tu ndizo zimeshiriki licha ya mashindano hayo kusimama kwa kipindi cha miaka nane sasa, ambapo mesema alitegemea kuona mwitikio mkubwa katika ushiriki wa Halmashauri hizo.
Aidha, amesema pamoja na Halmashauri hizo kushiriki bado hazijatoa washiriki waliotarajiwa na kushauri kuwa mashindano ya mwakani Halmashauri zijitahidi kutenga fedha kwa ajili ya mashindano ya SHIMISEMITA na kuongeza washiriki ili kuongeza ushindani wa mashindano hayo.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha mpira wa Netiboli Mkoa wa Morogoro Bi. Beatrice Selemani, ameeleza kuwa mashindano hayo yamekuwa na hamasa kubwa licha ya Halmashauri zilizoshiriki kuwa chache, ushindani ulikuwa wa hali ya juu kwa kuwa kila Halmashauri ilitaka kufanya vizuri na kuibuka na ushindi.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa wa Morogoro Bw. Angelus Likwembe amesema mashindano hayo yaliyozinduliwa Oktoba 26 mwaka huu, yatahitimishwa rasmi Oktoba 29 mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Angellah Kairuki (MB) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Jumla ya Halmashauri 144 kati ya 185, zimeshiriki mashindano hayo ya SHIMISEMITA ambayo yameshirikisha michezo lukuki ikiwemo Mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, riadha na michezo mingine mingi.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.