Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amezitaka Halmashauri zote nchini kuandaa utaratibu mahususi wa uuzaji na ununuaji wa viwanja utakaohusisha viongozi wa Halmashauri husika wakiwemo watendaji ngazi ya vijiji/mitaa ili kupunguza migogoro ya Ardhi inayoendelea kujitokeza.
Naibu Waziri ametoa kauli hiyo Julai 13 mwaka huu wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku ya pili Wilayani Morogoro kwa ajili ya kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi inayowakabili wananchi wa Manispaa hiyo.
Dkt. Mabula amesema endapo Viongozi wa Halmashauri wakiwemo Watendaji wake wakawa sehemu ya uuzwaji wa kila kiwanja ni wazi kuwa migogoro hiyo ya Ardhi itapungua au kuisha kabisa kwa kuwa kutakuwa hakuna udanganyifu baina ya pande mbili yaani mnunuaji na muuzaji baina ya pande hizo mbili.
“…Halmashauri andaeni utaratibu wa kuwa na fomu, kama kuna mtu ana eneo lake ndani ya Mji anataka kuliuza ni lazima pia nyie muwe sehemu ya uuzwaji wa eneo hilo ili kutambua hilo eneo ni mmiliki halali, mkiweka utaratibu huo hakuna mtu atauza eneo bila kufuata utaratibu. ….’’amesema Dkt. Mabula.
Katika hatua nyingine Dkt. Angelina Mabula amezitaka Halmashauri zote nchini kupitia upya kesi zote zinazohusu migogoro ya Ardhi ambayo inahusisha Watendaji wa Serikali na wananchi kuhakikiwa ili kupata ukweli halisi na kutoa haki kwa yule anayestahili.
RAS Morogoro Bi. Mariam Mtunguja akisikiliza kero za wananchi zinazotolewa mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula.
“…Niombe watumishi wa Halmshauri zote nchini, popote nitakapokuta kuna kesi ya mgogoro wa Ardhi baina ya kiongozi na mtu wa kawaida, na mtu wa kawaida umemkuta pale maana yake hiyo hati nitataka ibatilishwe…” amesema Dkt. Mabula.
Akizungumzia suala la urasimishaji wa Ardhi, Dkt. Mabula amempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu wananchi kurasimishiwa maeneo yao ambayo walijenga na kufanya makazi yao kwa muda mrefu huku akibainisha kuwa maeneno hayo hawatapewa wananchi ambao wamejenga hivi karibuni.
RC Morogoro Martine Shigela (kulia) na DC Morogoro Albert Msando wakisikiliza kero za wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na wananchi hao Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kutenga bajeti kwa ajili ya kupima maeneo yenye migogoro yakiwemo ya Kihonda na Mkundi ili katika maeneo hayo kila mwananchi atambue mpaka wake.
Aidha, Shigela amebainisha kuwa mara baada ya Manispaa kupima maeneo hayo wananchi watafikishiwa huduma zote muhim kiwemo huduma ya maji, ujenzi wa vituo vya Afya, soko, stendi ya mabasi na miundombinu ya barabara lengo ni kuwasadia wananchi hao kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuwa na changamoto zozote.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando, amempongeza Dkt. Angelina Mabula Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutatua kero ndani ya Wilaya hiyo na kumuahidi kutekeleza maagizo yote ambayo ameyatoa.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro Frank Mizikuntwe amewataka wanachi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuacha tabia ya kujenga maeneo ya milimani ili kutunza mazingira, kutunza vyanzo vya maji na taka ambazo zingezalishwa na wakazi wake na kusababisha bwawa la Mindu kupungua kina chake.
Wananchi wa Manispaa ya Morogoro wakiwa wamejipanga kuwasilisha kero zao kwa Mhe. Naibu Waziri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi walioshiriki Mkutano huo akiwemo Valentine Cosmas na Maria Michael wamesema migogoro mingi iliyopo katika halmashauri ya Manispaa hiyo inatokana na viwanja kuuzwa zaidi ya mara mbili (double allocation) ambapo husababishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali wasio waaminifu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.