Mhe. Fatma Mwassa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Wataalam wa mazingira Mkoani Morogoro wameshauri watu binafsi, taasisi, mashirika na kampuni binafsi nchini kujihusisha na biashara ya hewa ukaa kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaleta athari kwa binadamu.
Ushauri huo umetolewa Februari 23 mwaka huu na wajumbe mbalimbali walioshiriki kikao cha elimu juu ya biashara ya hewa ukaa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akifafanua juu ya dhana ya mabadiliko ya tabianchi, Mkurugenzi wa kituo cha Kitaifa cha kufuatilia Kaboni Prof. Eliakimu Zahabu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) amesema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto, ukame, mafuriko, n.k. huku akibainisha kuwa hayo yote yanatokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ovyo.
Aidha, Prof. Zahabu ambaye alikuwa ndiye mtoa mada mkuu wa kikao hicho amesema biashara ya hewa ukaa ni mfumo katika soko la dunia ambao unasadia kupunguza gesi joto angani ambayo inatokana na shughuli za viwanda na uchomaji wa moto na ukataji wa miti na uharibifu wa misitu iliyopo.
Mtoa mada prof. Eliakimu Zahabu akielezea kuhusu umuhimu wa biashara ya kaboni.
“...biashara hiyo inahusisha upandaji na utunzaji wa miti na kuweka mifumo inayodhibiti uzalishaji wa hewa hiyo katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kilimo, nishati, viwanda, na miundombinu...” amesema Prof Zahabu.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa baada ya mawasilisho na majadiliano ya mada mbalimbali zinazohusu biashara hiyo akaeleza maazimio ya kikao hicho, ikiwa ni pamoja na moja kati ya maazimio hayo ni kuundwa kwa kamati ya mazingira ya Mkoa ambayo itajishughulisha na utunzaji, uhifadhi na udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika Mkoa huo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kamati hiyo itakuwa chini ya mwenyekiti Mhe. Dkt. Julius Ningu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na itahusika na masuala ya biashara ya kaboni, uhifadhi na utunzaji wa wazingira kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Julius Ningu Mkuu wa Wilaya ya Ulanga ameteuliwa na Mkuu wa Mkoa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Mazingira ya Mkoa..
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amesema elimu waliyoipata kuhusu biashara ya kaboni ni fursa muhimu kwa serikali, watu binafsi, taasisi na wananchi kunufaika na mapato ya biashara hiyo pamoja na utunzaji wa mazingira na kupendekeza kuwa ili kufanikisha hilo, elimu inatakiwa itolewa kwa wananchi na viongozi ili kuwa na uelewa wa pamoja
Baada ya kikao hicho, wajumbe, waliazimia kuwa Halmashauri zote mkoani humo ziainishe misitu ya vijiji inayoweza kuingizwa kwenye biashara ya kaboni na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu biashara hiyo.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.