Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu ( Kazi Maalum) Captain mstaafu Mhe. George Mkuchika amesema Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) wamefanikiwa kupeleka huduma ya nishati ya Umeme katika Vijiji 652 kati ya vijiji 666 vya Mkoa wa Morogoro na kukamilisha huduma hiyo kwa vijiji vilivyobaki ifikapo Disemba Mwaka huu.
Mhe. kuchika amebainisha hayo Oktoba 28, 2024 wakati akiwasha umeme katika kijiji cha Magenge kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua, kuzindua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Serikali ya awamu ya sita katika Mkoa huo.
Aidha, Waziri Mkuchika amesema Serikali ya CCM inajukumu la kuhakikisha kero ya ukosefu wa umeme kuondoka ambapo Wilayani humo usambazaji wa nishati ya umeme umebakia vijiji 3 pekee vilivyobaki havijapata umeme hivyo ifikapo Disemba, Mwaka huu vijiji vyote vya Mkoa huo vitakuwa vimepata umeme.
".. Na hili la umeme nataka niwaambie wanagairo msiwe na wasiwasi ilani ya uchaguzi imesema hadi kufika Disemba Mwaka huu vijiji vyote viwe vimepata umeme..." amesema Mhe. George Mkuchika
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi ambapo katika kata ya Iyogwe imetoa shilingi Mil. 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya, Mil. 518 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari, Mil. 500 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji na Mil. 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na daraja ili kusogeza huduma muhimu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema katika Mkoa huo wenye jumla ya vijiji 666 ambapo vijiji 649 vimefikiwa kupata huduma ya umeme na vijiji 17 vipo katika hatua za ukamilishwaji ambapo matarajio ya Mkoa huo ni vijiji vyote 666 kupata huduma ya umeme ili kuanza kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji.
Naye Meneja wa TANECSO wa Wilaya ya Gairo Mhandisi Gilles Daniel akisoma taarifa ya Wilaya hiyo amesema kijiji cha Magenge ni moja kati ya vijiji nane katika Kata ya Madege ambapo mradi huo unagharamu ya zaidi ya Bilioni 5.4 hivyo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji vya Wilaya ya Gairo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.