Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akiwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Mkoa wa Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa leo Gairo.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameliagiza jeshi la Polisi pamoja na mamlaka nyingine wakiwemo ustawi wa jamii kubuni mbinu za kupunguza matendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kuweka mifumo madhubuti ya kiteknolojia ili kujenga Jamii Bora.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli (upande wa kushoto) akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame (upande wa kulia) wakiwa wanakalibishwa kwenye viwanja vya maadhimisho.
Mhe. Judith Nguli ametoa agizo hilo Machi 8 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Ambayo Kimkoa yamefanyika Wilayani Gairo katika viwanja vya Gairo A.
Maandamano na maadhimisho ya siku ya wanawake Wilayani Gairo ya kiongozwa na wakuu wa wilaya kutoka Gairo Mhe. Jabir Makame, Mvomero Mhe. Judith Nguli, Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka, Ulanga Mhe. Julius Ningu.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mvomero amesema, matendo ya ukatili wa kijinsia hayawezi kufumbiwa macho na Serikali kutokana na kuongezeka Kwa vitendo hivyo na kutumia fursa hiyo kuliagiza jeshi la Polisi pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kuongeza nguvu kukomesha vitendo hivyo.
"...niwaombe jeshi la Polisi na vyombo vingine vinavyohusika na Jambo hili kuhakikisha mnakuwa wabunifu, mnakuwa na mbinu ya kiteknolojia..." Amesema Mhe. Judith Nguli.
Sambamba na hilo, Mhe. Judith Nguli ameishauri jamii kuwachukulia hatua za kisheria familia zinazofanya vitendo hivyo vya ukatili katika familia zao, pia kuongeza ulinzi wa watoto na wanawake.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewashauri wanawake kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili vikundi hivyo ili wapatiwe mikopo kutoka kwenye Halmashauri zao ili waepukane na mikopo aliyoiita 'kausha damu' ambayo imekuwa ikiwatesa sana wanawake hao.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame aliye vaa kofia akitoa pongezi kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo yaliyo patikana kwenye awamu ya sita amesema hayo leo kwenye Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amesifu na kupongeza maendeleo yaliyopatikana hapa nchini Kwa kipindi cha miaka miwili chini ya Rais Mwanamke Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo kupitia Serikali yake wanawake wanatakiwa kujivunia kutokana mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mwanamke.
Aidha, amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha ukomavu wa kisiasa hapa nchini Kwa kitendo cha kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Wanawake wa Chama cha Demokrasia na maendeleo ( CHADEMA) na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha ukomavu na cha kihistoria katika nchi yetu.
Kwa upande wake Bi. Magreth Kapinga ambaye ni Afisa Hesabu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema wataendelea kuiishi kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa kuendelea kutumia teknolojia katika uzalishaji hasa katika shughuli za viwandani, maofisini na kilimo.
Bi. Magreth upande wa kushoto katika picha akiwa na akina mama kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani viwanja vya Gairo A
Bi. Magreth ameongeza kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia kumemfanya Mwanamke kuinuka kiuchumi.
Mandhari ya viwanja vya Gairo A
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.