Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Kadinali Polycarp Pengo amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima na kuzungumza mambo kadha wa kadha yanayohusu maendeleo ya nchi na watanzania kwa ujumla.
Askofu Mkuu Mstaafu Jimbo Kuu la Dar es salaam Kadinali Polycarp Pengo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima.
Mapema leo Agosti 9 mwaka huu, Mhasham Kadinali Polycarp Pengo aliwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake yalihusu ustawi wa jamii ya Morogoro na taifa la Tanzania.
Katika mazungumzo yao Mhasham Kadinali Pengo amesisitiza kutoruhusu dhana ya udini hapa nchini kwamba dhana hiyo inaweza kuiingiza nchi katika machafuko na kurudisha nyuma uchumi wa nchi na wa jamii.
Akigusia suala la uwekezaji wa bandari amesema suala hilo halihusiani kabisa na hoja ya Udini isipokuwa ni suala linalohusu maendeleo ya watanzania na taifa kwa ujumla.
“...nakumbuka mara ya mwisho niliongelea suala la Bandari nakuja kusikia wewe ni kwasababu ya udini...lakini basi mtu kama wewe utaelewa kwamba hii concern ilikuwa ni kwa ajili ya watanzania...“ amesema Kadinali Pengo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema viongozi wa dini hapa nchini wana nafasi kubwa ya kusaidia kutatua migogorondani ya jamii na kwamba kwa Mkoa wa Morogoro wanasaidia kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, hivyo amewashukuru viongozi hao na kuwataka waendelee kushirikiana na Serikali yao katika kuijenga jamii.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewapongeza viongozi wa dini kwa kuwa wavumilivu, wastahimilivu, wawazi na wenye busara katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima wakati akizungumza na Mhasham Kadinali Pengo.
Sambamba na hayo Mhe. Malima amewaomba viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kimsingi anafanya kazi nyingi za kimaendeleo na zote ni kwa ajili ya watanzania na Taifa hili.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya (kulia) akiwa pamoja na wasaidizi wa Mhasham Askofu Kadinali Pengo.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.