Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka wenyeviti wa Halmashauri za Mkoa huo pamoja na Wakurugenzi watendaji wa halmashauri, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha shilingi Bil. 4.7 zilizotolewa na Shirika la USAID kupitia mradi wa US AID Afya yangu unaolenga kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Kifua kikuu.
Dkt. Rozalia ametoa agizo hilo Disemba 10, 2024 wakati akishuhudia hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba baina ya Mtekelezaji Mkuu wa mradi wa USAID Afya Yangu (My Health) Deloitte Consulting Limited na Halmashauri za Mkoa wa Morogoro, hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Rozalia ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Uchumi na Uzalishaji Mali akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Mussa Ali Mussa amesema, lengo la Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutokomeza magonjwa ya VVU na Kifua Kikuu na akabainisha lengo la mradi huo kuwa ni kuimarisha utoaji wa huduma za afya ndani ya jamii kwa kuboresha uhusiano baina ya jamii na vituo vya Afya, hivyo amesisitiza matumizi sahihi ya fedha hizo.
".. Naomba kila mmoja wetu akatimize wajibu wake na suala la msingi niwasisitize matumizi sahihi ya hizi fedha kulingana na malengo yaliyotarajiwa.." Amesisitiza Dkt. Rozalia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa fedha na Utawala wa shirika la Diloitte Consulting Limited linalosimamia mradi wa USAID Afya Yangu Bw. Erick Mwelulila amesema, mradi huo unatekelezwa katika mikoa sita ya Iringa, Morogoro, Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma ambapo Mkoa wa Morogoro umepewa jumla ya shilingi Bilioni 4.7 zitakazotumika katika Halmashauri zote tisa kupitia mradi huo.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga ameishukuru USAID kwa kuja na mradi huo na kuiamini Serikali, hivyo amewataka viongozi wanaosimamia fedha hizo kuhakikisha wanazisimamia vizuri ili kuweza kujenga uaminifu huku akiahidi kwenda kutekeleza majukumu ipasavyo kama walivyoaminiwa na Shirika hilo.
Mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya zinazomlenga moja kwa moja mtumiaji, kuboresha uwezo wa mtu binafsi kuwa na tabia njema na kusaidia mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.