Mkoa wa Morogoro na Zanzibar imeendelea kukuza ushirikiano kwenye masuala ya kilimo hususan katika kilimo cha Karafuu na Mpunga ili kuongeza utaalamu kwa pande hizo mbili na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kupata masoko.
Hayo yalibainishwa Septemba 15, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akifunga ziara ya mafunzo ya Maafisa ughani mafunzo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa TARI wa kuoneshea teknolojia ya Kilimo uliopo Nanenane Mkoani Morogoro.
Mkoa umepokea maafisa 33 ambao wametembelea mashamba mbalimbali ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kilimo cha mazao mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ushirikiano wa pande hizo mbili ni muhimu kwani Morogoro inahitaji masoko ya mazao hususan Mpunga na Karafuu na Zanzibar inahitaji bidhaa hususan zao la mchele hivo ni vyema pande hizo mbili zikaongeza ushirikiano wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha upatikanaji wa mchele Zanzibar unaongezeka.
“Ninyi leo tunawakaribisha mjionee kama mpo sehemu ambayo katika mahusiano haya, mnatuhitaji na sisi tunawahitaji. Ninyi mna masoko, sisi tuna uzalishaji,”
amesema Mheshimiwa Adam Kighoma Malima.
Aidha amesema, Mkoa wa Morogoro kwa sasa ndio unaoongoza nchini kwa uzalishaji wa mchele, ambapo huzalisha tani 600,000 kwa mwaka wakati Zanzibar inazalisha tani 50,000 pekee huku uhitaji wake ukiwa tani 120,000 na kwamba ushirikiano huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mpunga visiwani humo kupitia mafunzo na mbinu bora zinazotumika katika Mkoa wa Morogoro.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amewaalika Maafisa hao ughani 33 kurudi Morogoro kufanya ziara kama hiyo hususan katika maeneo yaliyopo Mkoani humo yanayozalisha Mpunga kwa wingi ikiwemo Wilaya ya Kilombero na Malinyi maeneo ambayo hawakufika kwa sababu ya kuwa na siku chache za Ziara yao lengo ni kujifunza zaidi kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano (TARI), Dkt. Sophia Kashenge amesema, lengo la ziara hiyo ni kubadilishana uzoefu katika uzalishaji wa mazao mbalimbali na kubainisha kuwa TARI imeendelea kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARILI) katika kuboresha mbinu za kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuongeza tija na uzalishaji visiwani humo.
Dkt. Kashenge ameongeza kuwa ushirikiano huo hautaishia kwenye maneno pekee, bali utaendelezwa hadi kufikia hatua ya kuingia makubaliano ya maandishi, yenye malengo ya pamoja ya kuongeza uzalishaji kupitia tafiti mbalimbali za kilimo.
Naye Afisa Ughani Mkuu kutoka Zanzibar, Dkt. Salum Rehani, ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa kuwapokea na kuwapatia mafunzo hayo muhimu. Amesema wamejifunza mbinu mpya ya kitalu mkeka, ambayo haijaanza kutumika Zanzibar, na kwamba ujuzi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Afisa Uzalishaji kutoka Idara ya Umwagiliaji Maji, Bi. Rukia Mohamed, amesema wamejifunza umuhimu wa kutumia mbegu bora kulingana na misimu ya kilimo (vuli na masika), jambo ambalo awali halikuzingatiwa na kubainisha kwamba watayafikisha mafunzo hayo kwa wakulima wa Zanzibar ili waweze kutumia aina sahihi za mbegu na kwa msimu husika.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Adam Kighoma Malima alipata pia fursa ya kuzindua kisima cha maji cha kituo cha Uhaulishaji wa Teknolojia ya masuala ya kilimo - TARI, kilichochimbwa kwa ushirikiano na Serikali ya Mkoa ambacho kitarahisisha upatikanaji wa maji katika kituo hicho kilichopo Nanenane Manispaa ya Morogoro.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.