Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Denis Londo wakati wa kikao cha majumuisho baada ya ziara ya kukagua miradi ya TACTIC na ULGSP katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji Miji (TACTIC) na mradi wa uimarishaji miji Urban Local Government Strenghtening Programme (ULGSP) iliyotekelezwa Mkoani Morogoro na kutoa mapendekezo ya kuboresha miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge - TAMISEMI baada ya kamati hiyo kumtembelea Mkuu wa Mkoa kabla ya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi, wengine katika picha hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Denis Londo na Mhe. Margareth Sitta.
Mapema leo Oktoba 11 Kamati hiyo imefanya ziara na kukagua baadhi ya miradi ya TACTIC na ULGSP ikiwemo Soko kuu la Chifu Kingalu, Kituo cha dala dala cha Mafiga pamoja na kukagua barabara za nane nane na Tubuyu.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Denis Londo akizungumza wakati wa kikao cha majumuisho baada ya ziara ya kamati hiyo.
Akitoa mrejesho wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Denis Londo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mkoani Morogoro amesema kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi waliyoitembelea, na kuutaka uongozi wa Mkoa na Halmashauri kuendelea kusimamia miundombinu hiyo isiharibike.
Aidha, Kamati hiyo baada ya ziara yao imemuagiza Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima kuchunguza kwa kina suala la uuzwaji wa eneo karibu na soko kuu la Chifu Kingalu ambalo lilitakiwa kujengwa kituo cha dala dala ambacho kimejengwa Mafiga ili kubaini gharama na mhusika aliyekinunua eneo hilo.
“...sasa Mhe. Mkuu wa Mkoa Kamati inakuomba na inatoa rai ufanyike uchunguzi kuona ni mazingira gani yalipelekea Halmashauri kuuza lile eneo…...shilingi ngapi na zimeenda wapi...” amesema Mhe. Londo.
Sambamba na hilo, Kamati hiyo imeshauri Mkoa kuangalia namna ya kuwapunguzia waendesha piki piki (Bodaboda) ushuru wa kuingia kituo cha dala dala cha Mafiga ambao wanatozwa kiasi cha shilingi mia tano kila anapoingia.
Baadhi ya abiria wakisubiri magari katika Kituo cha dala dala cha Mafiga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima ameishukuru Kamati hiyo kwa ziara ya Kamati hiyo Mkoani humo na kuahidi kuwa Mkoa itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo ili kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo ya ULGSP na TACTIC.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza wakati wa kikao cha majumuisho cha kamati ya kudumu ya Bunge -TAMISEMI.
Nao baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge akiwemo Mhe. Margreth Simwanza Sitta Mbunge wa Jimbo la Urambo ameishauri Manispaa ya Morogoro kuanzisha vikundi vitakavyo shughulikia usafi wa barabara na mifereji ili iwe safi kuepusha mafuriko kipindi cha mvua kutokana na kuziba kwa mifereji hiyo.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Machela amesema Manispaa ya Morogoro ni moja ya Halmashauri ya miji 18 ambayo ilikuwa katika mpango wa utekelezaji wa mpango wa uimarishaji Miji “Urban Local Government Strenghtening Programme ikiwa na lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha miundombinu ya miji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii.
Mkurugenzi wa Halmashauri Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Machela akielezea hali ya utekelezaji wa miradi ya TACTIC na ULGSP katika Halmashauri hiyo.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo iliidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 49.6 na imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa soko kuu la Chifu Kingalu, kituo cha dala dala cha Mafiga, ujenzi wa barabara ya Barakuda kwa kiwango cha lami yenye urefu wa km 2.4, barabara ya Tubuyu km 2.4 na barabara ya Nanenane km 1.6.
Kamati hiyo iko kwenye zaiara ya kutembelea na kukagua miradi yaTACTIC na ULGSP katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Tanga na Arusha.
Hawa ni baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge -TAMISEMI.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.