Kamati ya Bunge yashauri wananchi Wilayani Mvomero kukubali kutumia mbinu kukabiliana na wanyama wakali
Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imewashauri wananchi wa Wilaya ya Mvomero wanaokabiliwa na changamoto ya kuvamiwa na Tembo, kuendelea kutumia mbinu zinazofundishwa na wataalamu ili kukabiliana na kadhia hiyo wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.
Afisa Wanyama Pori Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa (kushoto) akiwakaribisha Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela (katikati) na mgeni wake Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana kwenye eneo la mafunzo ya mbinu za kukabiliana na wanyama tembo kijiji cha Doma Wilayani Mvomero.
Ushauri huo umetolewa Juni 26 mwaka huu na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ally Makoa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini Wakati wa ziara yao Wilayani Mvomero kwa ajili ya kujifunza mbinu wanazotumia wananchi katika kukabiliana na tembo, mafunzo yaliyofanyika katika Kijiji cha Doma Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Ally Makoa akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo Mkoani Morogoro Juni 26 mwaka huu.
Mara baada ya mafunzo hayo, Kamati hiyo iligundua kuwa wananchi walio wengi Wilayani humo hawaoneshi mwitikio au nia ya dhati ya kujifunza mbinu hizo za kukabiliana na tembo hao zinazotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (TAWIRI) na kuwashauri kukubali kujifunza na kutumia njia hizo wakati Serikali inaendelea kutafuta njia sahihi na ya kudumu ya changamoto hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa kwanza kushoto) akiwa na Waziri wa Maliasili na utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati) wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Wizara hiyo Juni 26 mwaka katika kijiji cha Doma.
Wahe. Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo nao wametoa michangao yao ya mawazo pamoja na kupendekeza mbinu mbadala za muda katika kutatua kero hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa kama Darubini ya kuangalia mienendo ya tembo katika maeneo yenye kero, kuongeza magemu, pamoja na kujenga uzio wa umeme.
Dr. Emmanuel Masenga (aliyeshika kipaza sauti) ambaye ni mtaalamu kutoka TAWIRI akitoa mafunzo kwa Wahe. Wabunge juu ya namna ya kukabiliana na tembo pindi wanapovamia mashamba na makazi ya wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mhe. Fratei Gregory akijifunza moja ya mbinu za kukabiliana na tembo. picha ya juu mhe. amerusha kilipuzi na picha ya pili anajianda kulipua kilipuzi kingine .
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa tatu kushoto) akizungumza wakati wa mafunzo ya kukabiliana na tembo yaliyofanyika katika kijiji cha Doma Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Juni 26 mwaka huu wakati wa ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema suluhu ya kudumu ambayo inaendelea kufanyiwa kazi na Serikali ni kufanya upimaji wa maeneo yote ambayo ni mapitio ya wanayama hususan tembo hao yaani upimaji na kuyatambulisha kwa watanzania ili maeneo hayo yasiweze kutumika kwa matumizi yoyote ya shughuli za kibinadamu.
Kuhusu kifuta jacho na kifuta machozi kwa ndugu waliopatwa na maafa, Waziri Pindi Chana ameahidi kulifanyia kazi suala hilo huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kupeleka orodha ya wananchi wanaotakiwa kulipwa kifuta jacho na kifuta machozi hicho ili waweze kulipwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela pamoja na kuishukuru Kamati hiyo kutembelea Mkoani humo kwa lengo la kutatua kero ya uvamizi wa mnyama tembo katika Kijiji cha Doma na Wilaya ya Mvomero kwa jumla, yeye amejikita kuimarisha mawasiliano na mahusiano baina ya Maafisa wa Wanyama pori na wananchi wa maeneo yenye migogoro mingi ili pale wananchi wanapotoa taarifa basi wataalamu waweze kufika kwa wakati.
Naye Diwani wa Kata ya Doma Abdallah Elimu Kisuguru ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ameiomba Serikali pamoja na mbinu zote zinazoendelea kuwfundisha, ameishauri kujaribu kutumia mbinu ya wahenga wao ya kutumia magemu akiamini kuwa njia hiyo ndio itakuwa mwarobaini wa changamoto hiyo.
Akiwakilisha wananchi wenzake Mariam Mnamba ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugono amekiri kuwa pamoja na kutumia mbinu zinazofundishwa na wataalamu hao bado juhudi hizo hazijazaa matuda na tembo wameendelea kusumbua katika kijiji chake huku akimwomba Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwatazama kwa jicho la pekee kwani mwaka huu hawakupata mavuno yoyote kutoka mashambani mwao kwa sababu ya Tembo hao.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Antonia Antoni amesema, katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2021/2022 Wizara hiyo imepokea jumla ya taarifa 3,289 kupitia fomu za maombi ya kifuta jasho na kifuta machozi ambapo taarifa 3,256 zinazozungumzia uharibifu wa mashamba, 3 vifo vya mifugo, 11 watu kujeruhiwa na 19 vifo vya watu.
Wa kwanza kutoka kulia aliyeshika kipaza sauti ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Massanja akizungumza na wananchi wakati wa mafunzo ya mbinu za kukabiliana na wanyama wakali katika Kata ya Doma Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Aidha, amesema katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021 jumla ya shilingi 601,875,500 zimetumika kulipa familia za waathirika kama kifuta jasho na kifuta machozi.
Moja ya mbinu walizojifunza Waheshimiwa Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Ardhi na Maliasili ni pamoja na urushaji wa vilipuzi, matumizi ya oil chafu iliyochanganywa na pilipili, matumizi ya tochi, matumizi ya ving’ora mbinu ambazo wameonesha hawakuridhika nazo na kuitaka Serikali kuendelea kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na kukaa na wananchi kuwasikiliza mapendekezo yao.
Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasii na Utalii Mary Francis Masanja, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Ardhi Maliasili na Utalii Mhe. Ally Makoa, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dr. Pindi Chana, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, Diwani wa Kata ya Doma na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mvomero Abdallah Elimu Kisuguru pamoja na viongozi wengine wakikabidhi kwa uongozi wa Halmashauri ya Mvomero vitendea kazi vilivyotumika wakati wa mafunzo ya kukabiliana na tembo wanapoingia kwenye makazi ya watu au katika mashamba yao, Juni 26, 2022.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.