Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wameeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa skimu ya umwagiliaji ya Mgongola Wilayani Mvomero hivyo kuagiza kuuvunja baada ya mkandarasi wake kushindwa kukamilisha kwa wakati.
Kamati hiyo imetoa maagizo hayo Februari 16, Mwaka huu kupitia Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Mzuzuli (MB) kwa niaba ya Mwenyekiti na wajumbe wake walipotembelea skimu hiyo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yao Mkoani Morogoro.
Makamu Mwenyekiti huyo wa kamati amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 5.6, unahusisha hekta 620 zinazopata maji kutoka Mto Mkindo katika Kijiji cha Bungoma umekuwa ukisuasua kutokana na mkandarasi M/S BARD EAST AFRICA ENTERPRISES LIMITED aliyekabidhiwa mradi huo mwaka 2022.
"Mkataba huu unasimamiwa na sheria na mkandarasi ameshindwa kutekeleza wajibu wake, Tunapendekeza hatua zichukuliwe mara moja," alisema Mzuzule.
Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo amependekeza kuvunjwa kwa mkataba huo na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mkandarasi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anawajibika kwa hasara yoyote iliyojitokeza kwa wananchi na serikali.
Kwa upande wake, Mhandisi Ezra Chiwesela ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo (MB) amesema ucheleweshaji wa mradi huo umeibua changamoto kwa wakulima wa eneo hilo huku akiwataka watendaji wa serikali kushirikiana na viongozi wao wa ngazi za juu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango.
Kwa sababu hiyo, Menejimeti hiyo imeazimia kuvunja mkataba wa mkandarasi huyo baada ya kujiridhisha kutokuwa na nia njema na utekelezaji wamradi huo na kuwaathiri wananchi kiuchumi na kushindwa kufikia malengo yao.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema mradi huo una manufaa kwa Taifa zima ukilenga kuwa mradi wa mfano kwa Mikoa mingine hivyo Serikali haitafumbia macho jambo hilo na kuiomba Kamati hiyo kulighugulikia suala hilo.
Naye, Mhandisi wa umwagiliaji wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Mattanga Juma akitoa taarifa ya mradi huo amesema tayari ameshautolea taarifa ngazi za juu kuhusu kusuasua kwa mradi ikiwemo menejimenti ya Tume ya Taifa ya umwagiliaji kuiitisha vikao mara tatu kujadiliana na mkandarasi ili kunusuru mradi huo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.