Kamati ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yajipanga
Kamati ya maandalizi ya Maonesho ya wakulima - Nanenane Kanda ya Mashariki inayoundwa na Mikoa minne ya Dar es salaa, Pwani, Tanga na wenyeji Morogoro imeendelea na vikao vyake vya maandalizi ya Maonesho ya mwaka huu 2022 Mkoani Morogoro, lengo likiwa ni kufikia ufanisi mkubwa wa maonesho hayo kuliko miaka ya nyuma.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima wakati akiongoza kikao cha wataalamu na viongozi wengine kwa ajili ya maandalizi ya sherehe hizo kilichofanyika Mkoani Morogoro katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ukumbi wa Jeshi la Kujenga Taifa - JKT uliopo Nanenane.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akitoa wito kwa wananchi wa Kanda ya Mashariki mara baada ya Kikao cha Kamati ya maandalizi ya Kanda hiyo, kujitokeza na kushiriki Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu bora ya ufugaji, uvuvi na ukulima.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kupitia ushindani wa ndani uliopo baina ya Mikoa ya Kanda hiyo ya Mashariki itapelekea kujiandaa vema na kuhakikisha Maonesho hayo sio yatafana tu bali pia kushinda Kanda nyingine za Maonesho hayo na kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.
“Sasa ndio maana tupo kwenye vikao vya Kamati ili kuhakikisha tunapata utekelezaji Madhubuti kuweza kufikia malengo tuliojiwekea na hatimaye kushika namba 1 kitaifa” amesema Malima.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa Adam Malima ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga pamoja na Mikoa jirani kujitokeza kushiriki Maonesho hayo na kuchangamkia fursa za kupata elimu na teknolijia mpya za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi huku akiwataka wale wanaoleta bidhaa za maonesho kuleta bidhaa zenye ubora ili kunogesha maonesho hayo wakiwemo wanyama kama vile simba na wanyama wengine.
Baadhi ya vipando vilivyopo katika uwanja wa Maonesho wa MWL. J.K. Nyerere kama sehemu ya Maandalizi ya Maonesho hayo kwa mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya hiyo na Tanzania kwa ujumla kujitokeza na kufika katika Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kujionea jinsi wakulima wa mijini watakavyoweza kutumia ardhi kidogo ya kulima kwa tija.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albart Msando akipokea maelezo kutoka kwa Mkuu wa Idara ya kilimo wa Hamashauri ya Manispaa ya Morogoro Michael Waluse ya namna ya kutumia Ardhi kidogo kwa kilimo chenye tija.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Michael Waluse ameweka wazi kuwa kuna umuhimu wa wakulima kuweza kutumia teknolijia ya umwagiliaji kwa njia ya matone ya maji ili kuweza kutunza na kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi mengine ya kibinadamu lakini pia kuokoa gharama kubwa kwa mkulima.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi Kanda ya Mashariki ya Maonesho Nanenane kutoka Mikoa minne ya Morogoro, Tanga, Pwani na Dar es salaam wakiwa katika Kikao hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.