Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Morogoro imesema haijaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa barabara ya Ifakara - Mbingu Wilayani Kilombero uliotakiwa kuanza rasmi kutekelezwa Disemba 8, 2023 lakini hadi sasa bado unasuasua.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 29, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhandisi Joseph Masunga kwa niaba ya wajumbe wenzake baada ya kutembelea mradi huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yao ya siku tano kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho mkoani humo.
"...nieleze masikitiko yangu kutokana na mradi huu kususasua... barabara ndio kero kubwa katika maeneo ya huku..." amesema Mhandisi Joseph Masunga.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa imeelezwa kuwa changamoto kubwa ya mradi huo ni mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo kutolipwa malipo ya awali (Advance Payment) ambayo kimsingi ni haki yake kwa mujibu wa mkataba huo.
Kwa sababu hiyo, Mhandisi Masunga ameiagiza Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa kufuatilia kwa karibu changamoto hiyo na ili mkandarasi huyo alipwe na kuanza mara moja kwani amesema adha kubwa ya wananchi wa Mlimba ni uwepo wa ubovu wa barabara hususan wakati wa masika.
Hata hivyo, Mhandisi Masunga ameipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mlimba na kutumia fursa hiyo kuwapongeza watendaji wote wa serikali ngazi ya Mkoa, Wilaya na ngazi nyingine kwa kusimamia maono ya Rais.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima, amesema mradi wa Barabara ya Ifakara - Mbingu uko mikononi mwa TANROADS Makao Makuu na Mkoa hivyo ametaka kujipanga zaidi ili kuhakikisha mradi huo unaanza kutekelezwa mapema kwa manufaa ya taifa na usafirishaji wa mazao ya wananchi.
Naye Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Bw. Geofrey Mtakubwa amesema, mpaka sasa kazi zilizofanyika katika mradi huo ni upimaji, ujenzi wa kambi ya mkandarasi na kuleta vifaa 57 kati ya 137 ambapo ni sawa na 41.6% pamoja na kuleta wataalamu 7 kati ya 9 wanaohitajika.
Barabara hiyo yenye urefu wa km 62.5, inayojengwa kwa kiwango cha lami itakayogharimu shilingi Bil.97.1 inatekelezwa na mkandarasi M/S Henan Highway Engineering Group ya nchini China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ulitakiwa kuanza kutekelezwa Disemba 8, 2023 na kukamilika Juni 8 ,2026.
Mwisho
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.