Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro imeridhishwa na utendaji kazi wa Serikari ndani ya Mkoa huo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa Septemba 27, mwaka huu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Masunga wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya siku tano yenye lengo la kufanya tathmini ili kuona ubora wa miradi hiyo na hatua iliyofikiwa ukilinganisha na fedha zilizopokelewa (value for money).
Aidha, Bw. Masunga amesema, Serikali Kuu imefanya uwekezaji mkubwa kwa wananchi katika kutoa suluhisho la kiuchumi kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na mazao, kupata maji na matibabu kwa urahisi kazi hiyo inafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kulinda miundombinu ya umma ili idumu kwa muda mrefu likiwemo daraja la Luhembe Wilayani Kilosa.
"… niwaombe sana mshapata Daraja hili, naamini shughuli zenu zitaenda vizuri lakini mna hitaji kulitunza ili liweze kutumika kwa muda mrefu zaidi kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira hususan yanayozunguka Daraja …" amesema Bw. Joseph Masunga
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ili kuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwani amesema ni haki ya kila mtanzania kupiga kura ili kupata viongozi walio bora na watakaowaletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi kuacha kulima katika vyanzo vya maji kwani kufanya hivyo kunasababisha mito kubadili njia zao asilia, kuharibu miundombinu ikiwemo madaraja na Barabara badala yake amewataka kila mmoja kupanda miti ikiwemo minazi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kujipatia nazi kwa matumizi ya nyumbani.
Sambamba na hayo, Mhe. Malima amekemea vikali wakulima wenye tabia ya kuchoma miwa kwa makusudi ili kupewa kipaumbele katika kuuza miwa hiyo na kusisitiza kushirikiana kuwafichua wakulima wenye tabia hiyo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Nao wakazi wa Kijiji cha Kiberege Wilayani Kilombero akiwemo Bi. Rehema Kwanja wamefurahishwa na ujio wa kamati hiyo ya siasa huku wakiomba kuharakishwa kwa ujenzi wa majengo ya mama na mtoto ya hospitali ya Wilaya ya Kilombero ili kuepuka kufuata huduma hiyo mbali.
Siku ya kwanza kamati hiyo imeshatembelea miradi ya maendeleo katika Wilaya mbili za Kilosa na Kilombero, moja ya miradi hiyo ni Daraja la luhembe, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya ifakara Mji, Shule ya sekondari ya lipangalala, mradi wa maji na mradi wa Barabara ya Mkamba kwa kiwango cha lami.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.