Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Lazaro Londo ameutaka uongozi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa maslahi mapana ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.
Mhe. Londo amesema hayo Juni 24, 2023 akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati hiyo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya miundombinu ikiwemo ya ujenzi wa barabara zinazotekelezwa katika Halmashauri za Manispaa ya Morogoro na Morogoro vijijini Mkoani humo.
Amesema, ujenzi wa barabara ya Ngerengere - Mkulazi hadi Kidunda yenye urefu wa kilometa 70.54 inayounganisha vijiji vya kata za matuli, mkulazi- na ngerengere imeondoa changamoto ya kukosa mawasiliano kwa wakazi wanaoishi katika maeneo hayo.
"... tuharakishe miundombinu ikiwemo Barabara hii ambayo ni uthibitisho wa Serikali kuwaunganisha wananchi wetu kimawasilino ya shughuli za kiuchumi na kijamii zikiwemo shughuli za mashambani kwenda sokoni kwa ajili ya kupeleka mzao yao" amesema Mhe. Londo
Aidha, amepongeza maamuzi ya TARURA ya kujenga barabara katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuwakwamua wananchi kiuchumi hasa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Sambamba na maagizo hayo amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea Bajeti TARURA kwani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bajeti ya TARURA imeongezeka kwa Shilingi Bil.350
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendelea kuisimamia TARURA pamoja na kuyafanyia kazi maelekezo ya kamati na ushauri walioutoa kwa maslahi mapana ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Nsemwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameishukuru kamati hiyo kufanya ziara Wilayani humo na kwa niaba ya watendaji wa Serikali Wilayani humo amesema ameyapokea maelekezo ya Kamati hiyo na watayatekeleza.
Kamati hiyo imehitimisha ziara yake Mkoani Morogoro ambapo miradi mbalimbali imekaguliwa ukiwemo ujenzi wa Daraja la Berega la Wilayani Kilosa lenye urefu wa mita 140.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.