Kamati ya Ukaguzi RUWASA yatoa maagizo.
Kamati ya Ukaguzi ya Wakala wa Usambazaji maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeagiza kuharakishwa upatikanaji wa vifaa vya kuchuja maji katika mtambo wa Uzalishaji maji uliopo Wilayani Gairo ili mtambo huo uweze kurudi katika hali yake ya uzalishaji wa kawaida na kuwaondolea wananchi wa Gairo kero ya maji.
Mwenyekiti wa ufundi na Miradi (RUWASA) Mhandisi Ngwisa Mpembe akitoa maagizo kwa RUWASA Wilaya ya Gairo wakati wa ziara yake ya kukagua Miradi ya maji Julai 12 mwaka huu.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro Bw. John Msengi akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa ufundi na Miradi (RUWASA) Mhandisi Ngwisa Mpembe Julai 12, 2022 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ambayo imetembelea Miradi ya maji katika Wilaya za Gairo na Kilosa Mkoani Morogoro.
Wanakamati wa Bodi ya ufundi ya RUWASA wakiwa katika Kikao cha ndani wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Baada ya kutembelea Mtambo wa uzalishaji Maji Gairo Mjini Kamati hiyo imeshuhudia mtambo huo wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja na laki nane kwa siku (1,800,000) ukiwa umeshuka kiwango cha uzalishaji wake kwa asilimia 50 kutokana na mashine moja kufanya kazi badala ya mbili.
“Mtambo huu unauwezo wa kuzalisha lita milioni moja na laki nane (1,800,000) kwa siku, lakini kwasababu za kiufundi sasa hivi uzalishaji umeshuka kwa karibia asilimia 50, kwa hiyo kama bodi tumeiagiza mamlaka chini ya usimamizi wa meneja wetu wa Mkoa kwanza kuharakisha kufanya kila liwezekanalo vifaa hivyo ambavyo ni membrane vifaa vya uchujaji vipatikane haraka” amesema Mhandisi Mpembe.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji RUWASA Gairo Evance Mangosho amesema serikali imeshatenga bajeti ya Shilingi Milioni mia moja na hamsini {Tsh.150,000,000/=} kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo na wanatarajia mwezi wa tisa mwaka huu vifaa hivyo vitawasili kutatua tatizo hilo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa RUWASA Gairo Evance Mangosho akiwaelekeza wanakamati wa RUWASA namna mitambo hiyo inavyofanya kazi.
Baadhi ya mitambo inayomilikiwa na RUWASA Wilaya ya Gairo.
Naye Jumanne Raymond ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mapilipili B Wilayani Kilosa kwa niaba ya wananchi wake ameishukuru Serikali Pamoja na RUWASA kwa kuwaondolea changamoto ya maji katika eneo lake na kuwaomba kuendeleza usambazaji katika maeneo mengine ambayo haya japata Maji.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi John Msengi amesema kuwa, wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo kwa lengo la kuimarisha Zaidi upatikanaji wa maji safi na salama kwa Wananchi.
Miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo katika wilaya hizo ni Mradi wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Gairo, Mradi wa jumuiya ya watumia Maji Berega Pamoja na Mradi wa maji Rudewa Wilayani Kilosa ambao inatekelezwa kwa fedha za UVIKO 19.
Baadhi ya wananchi wakifurahia huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama Wilayani Gairo na Kilosa.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.