Wajumbe wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamebariki mazungumzo yanayoendelea baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Wizara ya Biashara Zanzibar kupitia Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (Zanzibar State Trading Co - Oparation – ZSTC) kuwa na ushirikiano wa kufanya biashara ya zao la karafuu inayozalishwa Mkoani Morogoro.
Kauli hiyo imetolewa Novemba 14, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bi. Mtumwa Pay Yusuph alipofanya ziara ya siku moja Mkoani Morogoro yeye na Wajumbe wake kwa lengo la kujiridhisha uhalisia wa mazungumzo yanayoendelea.
Akizungumza mara baada ya kutembelea ghala la karafuu la Tawa lililopo Matombo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na maeneo yanayozalisha Karafuu na kuona mwamko mkubwa wa wakulima katika kulima zao hilo, Wajumbe waliridhika na hali ya uzalishaji wa zao hilo hivyo kutoa baraka ya kuendeleza na mazungumzo kwa pande hizo mbili.
“tumezunguka katika maeneo tuliyoyatarajia ambayo wenzetu wa ZSTC wameshafanyia mazungumzo, tumekwenda kuliona na hilo ghala lenyewe Kwa kweli tumeona, mikarafuu ipo na wakulima wapo na miche mingi wanazalisha”
Katika Hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ameziomba Serikali za pande zote mbili kukaa chini na kufanyia utekelezaji wa mazungumzo yaliyoazishwa na pande hizo mbili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima mara baada ya kuwapokea wageni wake hao Ofisini kwake, aliwathibitishia wajumbe hao kuwa kama wataendelea kujipanga kwa Pamoja baina ya pande hizo mbili na kufanyia kazi mipango yote iliyopangwa, kuna uwezekano mkubwa Tanzania kuwa namba mbili Duniani katika uzalishaji wa zao la Karafuu.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameelezea mkakati wa kuendeleza zao la Karafuu ndani ya Mkoa huo na kubainisha kuwa programu ya Mkoa katika kuharakisha kukua kwa zao hilo ni kununua miche ya karafuu inayooteshwa na wakulima wenyewe na kisha kuigawa bure kwao, lengo ni kuleta hamasa zaidi katika kilimo cha zao hilo.
Aidha wajumbe wa Kamati hiyo walitoa ushauri mbalimbali wa nmna ya kulima zao hilo kulistawisha kitaalamu na kwa kufanya hivyo kutapelekea kupata karafuu iliyobora na kuendeleza sifa ya zanzibara kutoa karafuu bora na Dunianii
Wakisoma Risala mbele ya mwenyekiti wa Kamati , kikundi cha Tugende kilichopo Kijiji cha Kibwaya kata ya Mkuyuni wametaja lengo la kuanzisha kikundi hicho kuwa ni kuhamasisha uzalishaji wenye tija wa mazao ya viungo katika milima ya Ulugului na kutunza mazingira, vyanzo vya maji na kuongeza kipato kwa wanakikundi.
Wanakikundi hao walibainisha kuwa walianza kuzalisha miche ya karafuu 2,800 mwaka 2019, 2020 miche 4,600, mwaka 2021 miche 12,000, 2022 miche 16,000, mwaka 2023 walizalisha miche 38,000 na mwaka 2024 wamezalisha mechi 68,000 huku matarajio ya mwaka 2025 ni kuzalisha miche 100,000.
Hata hivyo wametaja changamoto inayowakabili kuwa ni mabadiliko ya tabaichi inayosababisha mvua zisizo za uhakika hivyo wameiomba Serikali kuwasadia kuwa na miundombinu ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha mazao hayo ya viungo hususan zao la karafuu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.