Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kasi ya maambukizi mapya ya UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 4.5 miaka sita iliyopita hadi asilimia 3.3 mwaka 2024 kutokana na juhudi kubwa za kamati ya afya inayoundwa na idara mbalimbali za afya na wadau mbalimbali wa Mkoa huo.
Mhe. Malima amesema hayo Novemba 13, Mwaka huu wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vya kutolea huduma katika sekta ya afya Mkoani Morogoro vyenye thamani ya Tsh. Mil. 52 aambavyo vimetolewa na shirika linaloshughulikia afya ya familia ya kimataifa (FHI 360) kwa kushirikiana na watu wa marekani (USAID) katika mradi wake (Epidemic Contro - EPIC) ukiwa na lengo la kupunguza na kuondoa maambukizi mapya ya UKIMWI hapa nchini.
Akifafanua zaidi, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa maambukizi ya UKIMWI yaligundulika mwaka 1988 mpaka sasa ni zaidi ya miaka 36 na kwamba Elimu zinazotolewa kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo imesaidia kutambua njia za kuzuia maambukizi mapya na walioambukizwa tayari wanapata usaidizi wa mapema kwa kupatiwa mahitaji muhimu ikiwemo dawa ili kuwa na afya bora.
“… kasi imepungua kutoka 4.5% hadi 3.3% sio ndogo kwani kuna kitu tunachofanya ambacho kipo sawa sawa ndio maana maambukizi yanashuka…” amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Aidha, Mhe. Malima amesema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia utafiti uliofanyika kuonesha kuwa mama mjamzito mwenye maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu anaweza kujifungua mtoto asiye na maambukizi.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wadau mbalimbali wa sekta ya afya Mkoani Morogoro kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa wa UKIMWI ili kufikia lengo la chini ya asilimia 2 au kuuondoa kabisa baada tathmini itakayofanyika tena miaka sita ijayo kwani kutokuwa na ugonjwa wa UKIMWI Mkoani humo inawezekana.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa huyo amelipongeza shirika hilo kwa kutoa misaada hiyo kwa sekta ya afya ili kuendelea kutoa huduma hiyo kwa haraka.
Kwa upande wake, meneja wa mradi wa EPIC Mkoa wa Morogoro Bw. Azizi Itaka amesema mradi huo unatoa huduma kwa Mikoa 11 ikiwemo Morogoro lengo likiwa na kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI kwa kutekeleza afua tatu muhimu zikiwemo kutoa elimu ya kujikinga na virus vya UKIMWI, kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia na kufanya upimaji wa ugonjwa huo na kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya ngono katika jamii na wakishagundulika kuathiriwa wanafanyiwa utaratibu wa kufika sehemu sahihi kwa ushauri na tiba kamili.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma amelishukuru shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada huo katika sekta ya afya ili kuongeza nguvu katika kuhudumia wananchi wanaopata maambukizi mapya ili kuwa na afya bora kama watu wengine.
Mradi wa EPIC ulianza 2020 – 2025 ukisimamiwa na serikali ya watu wa Marekali USAID ambapo wametoa vifaa mbalimbali vikiwemo makabati, mabegi, pamba, sindano, glovu za mikono, makoti, viatu na sanduku za kubebea vifaa mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma Mkoani Morogoro.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.