Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi Dk. Allan Kijazi ameuagiza Uongozi wa Mkoa wa Morogoro kufanya upya tathmini ya wadaiwa sugu wa mashamba makubwa Mkoani humo ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki wa mashamba hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dr. Allan Kijazi akisikiliza na kutatua chcngamoto za watumishi wa Idara ya Ardhi Mkoa wa Morogoro, Juni 3 mwaka huu alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja.
Dk. Kijazi ametoa agizo hilo Juni 3 Mwaka huu wakati wa ziara yake ya Kikazi ya siku moja Mkoani humo ambayo pamoja na mambo mengine, ilikuwa na lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za watumishi wa Idara ya Ardhi pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Anza-amen Ndossa akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dr. Allan Kijazi ili azungumze na Maafisa wa Idara ya Ardhi.
Katibu Mkuu katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa, ameweka wazi kuwa kitendo cha baadhi ya wamiliki wa mashamba makubwa kutolipa madeni ya kodi ya pango la umiliki wa ardhi ni kuikosesha Serikali mapato halali na hivyo kuisababishia Serikeli hasara.
“Kwanza tupate takwimu kamili ya madai ya mashamba yote makubwa kwa Mkoa wa Morogoro, madeni tunayowadai ili tuweze kuchukua hatua mahususi kuhusu wamiliki wa mashamba haya” amesema Dk. Kijazi.
Sambamba na hayo Dk. Kijazi ameonya utaratibu wa wananchi kuvamia mashamba na maeneo yaliyowazi au yasiyoendelezwa na baadae kuomba kupewa mashamba hayo ambapo baadhi ya wananchi huishia kuyauza maeneo hayo. amesema, utaratibu huo hautakuwa na tija katika Taifa na hivyo Serikali inalazimika kukemea tabia hiyo na kuchukua hatua kali ili kulinda ardhi kwa manufaa mapana ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Anza-amen Ndossa amemuomba Katibu Mkuu huyo kusimamia kikamilifu matumizi ya ardhi ya Mkoa huo kwani Mkoa wa Morogoro kiuchumi na kimaendeleo unategemea ardhi kwa zaidi ya 90% kupitia kilimo na ufugaji hivyo kuendelea kuwa na migogoro ya ardhi Mkoani humo ni chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wa Mkoa huo na taifa kwa jumla.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe amemuomba Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kibali cha kutoa hati miliki za kimila kwa kutumia mfumo wa zamani ili kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi iliyopo baina ya mtu na mtu au jamii na jamii Mkoani humo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Ally Machela ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuikopesha fedha Halmashauri hiyo kwa ajili ya zoezi la kupima viwanja katika maeneo ya Kata ya Kihonda upande wa Kiegea STAR CITY ili kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka ambapo hadi sasa zaidi ya viwanja 3600 vimepimwa kupitia mkopo huo.
Afisa Ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Edward Lugakingira kwa niaba ya maafisa Ardhi wa Mkoa huo amebainisha kuwa bado kwa baadhi ya Halmashauri hazina Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya hali inayosababisha wananchi kufuata zaidi ya umbali wa 174Km kufuata huduma ya utatuzi migogoro ya ardhi katika Wilaya jirani hivyo kuongeza gharama kubwa kwa wananchi.
Katibu Mkuu Dr. Allan Kijazi akiwa katika picha ya pamojana watumishi wa idara ya ardhi Mkoani Morogoro baada ya kumalizika kwa mkutano wake na watumishi hao Juni 3 mwaka.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.