KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS AHIMIZA UPANDAJI MITI
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mary Maganga ameitaka jamii kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika maeneo yao na kutunza uoto wa asili ili kupunguza gesi joto (Hewa ukaa) inayosababishwa na ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Katibu Mkuu Mary amesema hayo Februari 23 mwaka huu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa REDD+, hafla iliyofanyika Cate Hotel iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi Katibu Mkuu huyo amesema mradi huo una lengo la kuhifadhi uoto wa asili na misitu ambayo kwa sasa imeathiriwa na shughuli za kibinadamu na kupelekea hewa ukaa kuongezeka na kwamba suluhisho lake ni kupanda miti.
“Lakini wewe na mimi tukipanda miti katika maeneo yetu ya makazi, wewe na mimi tukitunza uoto wa asili tutaleta mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu” amesema.
Aidha, amesema kikao hicho kinalenga kuzijengea uwezo zaidi taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinahusiana na masuala ya uhifadhi ili kuweza kutekeleza mradi huo kwa ufanisi zaidi yakiwemo mazingira ya Mkoa wa Morogoro ambayo uoto wake umeharibiwa sana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mzingira Dkt. Andrew Komba, amesema zaidi ya hekta laki Nne za Misitu zinakatwa kwa mwaka hivyo kusababisha hewa ukaa kuongezeka hali ambayo amesema kama haitadhibitiwa italeta athari zaidi hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) Geoffrey Kilenga amesema mradi huo unalenga kuendeleza kilimo rafiki yaani shughuli za uzalishaji hususan kilimo zinakuwa endelevu na zenye tija lakini bila kuharibu mazingira.
Mradi wa REDD+ kwa sehemu kubwa unafadhiriwa na Serikali ya Norway na ni moja ya jitihada za Serikali katika kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi hivyo kupunguza madhara yake ikiwa ni pamoja na ongezeko la ukame, mafuriko ya mara kwa mara uhaba wa chakula na maji pamoja na kuyeyuka kwa seruji kwenye milima mirefu.
Imefahamika kuwa Mradi huo wa REDD+ hadi kukamilika kwake, utagharimu takribani dola za Marekani milioni mia tatu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.