Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoani Morogoro Bi. Beatrice Njawa amewaagiza Wakuu wa idara ya viwanda, biashara na uwekezaji wa Halmashauri za Mkoa huo kugawa majukumu yao kwa Maafisa walio chini yao ili kutokwamisha utendaji kazi wa Serikali katika Halmashauri zao.
Bi. Beatrice ametoa wito huo kwa Maafisa hao Septemba 5 mwaka huu wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha kupeana uzoefu wa kiutendaji na kilichoshirikisha Wakuu wa Idara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro.
Akihitimisha Kikao hicho kilichofunguliwa Agosti 4, 2023 na Katibu Tawala wa Mkoa huo Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji amekitaka kikao hicho kiwe na matokeo chanya hususan katika masuala ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na masoko.
Aidha, amewataka Viongozi wa ngazi hizo za Wilaya kuwasilisha taarifa zao za kazi zilizofanyika kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni za Kiserikali.
"... utekelezaji wa majukumu ni muhimu zaidi hivyo taarifa hizi ziwasilishwe kila baada ya robo mwaka na mnatakiwa kufanya mgawanyo wa majukumu kwani inawezekana mtu mmoja akawa anafanya vitu vingi wakati wengine wapo..." amesema Bi. Beatrice Njawa.
Aidha, amesema, pamoja na majukumu yao pia wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara hususan sekta binafsi na kuweza kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita ya inayoongoza na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wao, Maafisa biashara akiwemo Bw. Mohamed Kinuga kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi amesema kikao hicho kimewapa Elimu ambayo hawakuwa nayo kabla yake ikiwemo Elimu ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo ameahidi kwenda kuwashawishi wakulima kutumia mfumo huo ili kujipatia bei inayoendana na thamani ya mazao wanayouza.
Mwisho.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.