Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameitisha kikao cha dharura Mkoani humo kwa ajili ya kuweka mikakati ya matumizi ya fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 walizopata kutoka Serikalini.
Martine Shigela ameitisha kikao hicho Oktoba 17 mwaka huu kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa CCT Kilakala katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kushirikisha wataalamu mbalimbali wa Halmashauri pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama ndani ya Mkoa huo.
Wakati wa ufunguzi, Martine Shigela amesema, kikao hicho sio cha kiitifaki bali ni kikao kinacholenga Mkoa kuweka mikakati ya kwenda mbele katika kutekeleza kwa ufanisi matumizi ya fedha zaidi ya Tsh. Tril. 1.3 alizotafuta Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za Kupambana na Uviko – 19 na Mkoa kupata mgao wa zaidi ya Tsh. 19.9 Bil.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Mkoa ameelekeza kwa sasa kuanza na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za Msingi na Sekondari ili kutowakosesha wananfunzi masomo yao ifkiapo Januari mwakani na kuwataka kila Halmashauri kukamilisha majengo hayo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
“Ningependa ikiwezekana kabla hata ya tarehe 15, tarehe mbili, tatu Nne ya Disemba tuanze kuona majengo ya madarasa ya wanafunzi wetu yamekamilika” ameagiza Shigela.
Pamoja na maagizo hayo amewataka Wakurugenzi pamoja na wataalamu wao kubaki vituoni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo kama walivyokubaliana kwenye kikao na kwamba hategemei kuona kiongozi wa Halmashauri kuondoka eneo lake la kazi kabla ya kukamilisha kazi hiyo.
“kama mimi Mkuu wa Mkoa siondoka, sitarajii mtu mwingine ataondoka kabla ya kukamilisha hii kazi, naomba sana, naongea kistarabu tena kwa kuwaomba, kipimo chetu ni kazi hii” amesisitiza Shigela.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo kutoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kila Ijumaa ya kila wiki na Oktoba 22 wawasilishe taarifa ya kuwapata mafundi na taratibu za manunuzi wa vifaa vya ujenzi ili Mkoa uanze mchakato wa kuagiza vifaa hivyo kiwandani kama walivyokubaliana kuwa manunuzi ya vifaa hivyo yatafanyika kwa pamoja kimkoa ili kupunguza gharama.
Hata hivyo Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Mariam Mtunguja amefafanua suala la ununuzi wa vifaa vya ujenzi kuwa bado hilo ni jukumu la Wakurugenzi, katika kila hatua inayohitajika ya manunuzi kwa kufuata taratibu za manunuzi, Mkoa utahusika kwenye utaratibu pekee na kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa gharama nafuu.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando yeye alishauri kuwa pamoja na uharaka na muda mfupi uliopo, ni muhim manunuzi hayo yasikiuke taratibu za kimanunuzi ili Mkoa usiweze kuingia kwenye mtego wa matumizi mabaya ya fedha wakati wa ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo.
Huku Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mhe. Innocent Kalogeresi ameshauri wataalamu katika ujenzi huo wa madarasa kujaribu kuona namna nyingine mbadala ya kupunguza gharama hususan katika matumizi ya matofali ya kuchoma.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamis Tale Tale akiwasilisha taarifa kwa wajumbe wa kikao hicho.
Aidha, wajumbe wengine wakiwemo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama akiwemo mwakailishi wa Jeshi la Magereza Moa wa Morogoro, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuagiza kikao hicho kufanyika mapema huku akiwatoa wasiwasi wajumbe wa kikao hicho kuwa Jeshi la Magereza Mkoani humo lina uwezo wa kufanya kazi ya kujenga madarasa ndani ya Mkoa huo kwa ufanisi endapo litapewa ridhaa hiyo kama ilivyopendekezwa na wajumbe wa kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Morogoro waliohudhuria katika kikao hicho.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Mkoa wa Morogoro Bw. Anza Amen Ndosa alifafanua namna fedha zaidi ya Tsh. 19.9 Bil. zilizotolewa na Serikali zitakavyotumika Mkoani humo kuwa Tsh. 630,000,000/= zimelenga kujenga nyumba za watumishi, Tsh. 1.2Bil. zitatumika kununua X - ray na Tsh. 100Mil. Kujenga vyumba vya wagonjwa mahututi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja (kulia) akiteta neno na Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Mipango na Uratibu Anza Amen David Ndossa wakati wa kikao hicho.
Fedha nyingine ni Tsh. 900Mil. zitajenga majengo ya huduma za Dharura, Tsh. 80Mil. zitajenga miundombinu ya shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum Wilayani Mvomero, Tsh. 2,840,000,000/= zitajenza vyumba vya madarasa katika vituo shikizi na Tsh.14,140,000,000/= zitajenga madarasa ya shule za Sekondari na kufanya jumla ya fedha zote Bil. 19,950,000,000/= kuwa zitatumika.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.