Mwenge wa Uhuru 2022 wapongeza Mradi wa Maji unaotekelezwa Kilosa/RUWASA
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2022 Bw. Sahili Gereruma ameipongeza Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kwa kutekeleza ipasavyo Mradi wa Maji wa Rudewa unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na hivyo kuunga mkono sera ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichawani.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 25 ikiwa ni siku ya pili ya Mwenge wa Uhuru kukimbizwa Mkoani Morogoro na leo ukiwa Wilayani Kilosa ambapo umepitia jumla ya miradi mitano ukiwemo mradi wa maji Rudewa ambao unaonekana kuwavutia wakimbiza Mwenge kutokana na mradi huo kujengwa kwa kiwango kinachokubalika.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa (Sahili Gereruma )Katikati
“ndugu zangu wana Rudewa, mwenge wa uhuru umefika hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wetu wa maji unaotekelezwa na ndugu zetu wa RUWASA, kwenye hiki kipengere cha maji RUWASA mko vizuri, hongereni sana” Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru amepongeza.
Mwenge wa Uhuru unavyoleta ,matumaini na kuchochea maendeleo
Aidha, baada ya kutoa pongezi hizo kwa wote walishiriki kutekeleza mradi huo wa maji Kiongozi huyo wa mbio za mwenge amewataka kuendelea kuwa waaminifu na kumalizia maeneo madogo ambayo yamebakia kumaliziwa kwenye mradi huo.
Katika hatua nyingine Bw. Geraruma amewaagiza wanaotekeleza mradi huo kumalizia kwa wakati ikiwa ni pamoja na kujengea uzio vituo vyote vya kuchota maji huku akiwataka wananchi wa Rudewa na wengine hapa nchini kuwa na utamaduni wa kuvuta maji katika nyumba zao akisisitiza kuwa hiyo ndio maana halisi ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi 3.1 Bil. Kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Maji ndani ya jimbo hilo ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Rudewa ambao umegharimu kiasi cha takribani shilingi milioni 847.
Katika hatua nyingine Prof. Paramagamba Kabudi amewataka wananchi wa Jimbo la Kilosa kutunza misitu kwa kuwa ndio vyanzo vya maji yote wanayotegemea huku akiwasihi kutokata miti ili miti hiyo iweze kusaidia kutunza vyanzo vya maji hayo.
Taarifa iliyotolewa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa imeleza kuwa lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya maji mengi, safi na salama kwa saa 24 kwa wakazi wapatao 13,516 wa kata ya Rudewa Wilayani Kilosa na kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi hao kutoka 15% hadi 95%.
Mwenge wa Uhuru umekamilisha mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa salama wasaalimini na kesho mwenge huo utaendelea kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.