Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amelishauri Shirika la Germany TB and Leprosy Relief Association ( GLRA) linalojishughulisha na ugonjwa wa ukoma, kujikita katika kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo ili kuzuia maambukiza mapya ya ukoma kwa jamii, kwa kuwa amesema KINGA NI BORA KULIKO TIBA.
Dkt. Mussa amesema hayo Septemba 26, 2024 wakati akizindua mpango wa kutokomeza ugonjwa wa Ukoma Mkoa wa Morogoro, uzinduzi uliofanyika katika Hoteli ya Morena iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, programu mbalimbali zinazoanzishwa huwa hazizungumzii sana suala la kuzuia bali huzungumzia masuala ya kutibu hivyo amewataka wataalamu hao kuwa na mpango mkakati wa kuzuia kuenea kwa Ugonjwa huo wa ukoma.
".. kuna haja kwa sisi wataalamu tuendelee kusisitiza kutafuta mbinu ya namna gani ya kuweza kufanya Prevention ya haya maradhi.."Amesisitiza Dkt. Mussa
Aidha Dkt. Mussa amesema Mikoa ya Morogoro, Mtwara, Lindi, Tanga na visiwa vya Unguja ndio inasemekana ina visa vingi vya ugonjwa huo, hivyo amelitaka shirika hilo kuweka mkazo katika maeneo hayo ili kusaidia kujua chanzo cha kuenea kwa Ugonjwa huo.
Sambamba na hayo amelitaka Shirika hilo la GLRA kuwatumia wataalamu wa Afya walioko ngazi ya chini kwa lengo la kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wenyewe hivyo kusaidia kutoenea katika ngazi za chini.
Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Taifa wa TB na Ukoma Dkt. Liberate Mleoh amesema programu hiyo ni mahususi kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Ukoma lengo ni kwamba ifikapo 2023 kusiwe na maambukizi ya Ukoma.
Aidha, katika kikao hicho imebainishwa kuwa programu hiyo kwa Mkoa wa Morogoro inatekelezwa katika Wilaya tatu za Halmashauri ya Mlimba, Ifakara Mji na Manispaa ya Morogoro, huku wito ukitolewa kwa Wananchi kutoa taarifa kwa wataalamu wa afya pindi mtu atapojihisi ana ugonjwa huo.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mlimba Dkt. Deodati Jumanne akiongea kwa niaba ya waganga wa Halmashauri za Ifakara Mji na Halmashauri ya Manispaa amesema, mpango huo wameupokea na wapo tayari kuutekeleza ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.