KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGEZA WA UHURU KITAIFA ATAKA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA USALAMA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma amewataka wananchi wa Kiberege Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro na watanzania wote kwa jumla kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama pale ambapo wanahitajika ili kujenga taifa la Tanzania linalosifika kama kisiwa cha Amani.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi (kushoto) akikabidhi risala ya Utii ya wananchi wa Wilaya hiyo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 mara baada ya kusomwa na Katibu Tawala wake kwa niaba yake
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi (kulia) akiwa katika picha ya makabidhiano ya Mwenge wa uhuru mara baada ya kuingia Wilayani kwake. kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Adam Bibangamba
Ndugu Sahili Geraruma ametoa kauli hiyo leo Agosti 29 wakati akifungua kituo cha Polisi cha Kata ya Kiberege Wilayani humo ambako Mwenge wa uhuru umekimbizwa kwa Km 183 na kupitia miradi sita yenye thamani ya zaidi ya shilingi 1.1 Bil.
Moja ya miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru 2022
Akiwa katika Kituo cha Polisi cha Kata ya Kiberege Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amesema wananchi hawana budi kukitumia kituo hicho cha polisi kama kimbilio lao mara wanapopata matatizo yanayohusiana na polisi na kwamba wanatakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Polisi ili kudumisha Amani katika kata yao na Taifa kwa jumla.
“sambamba na hilo wanakiberege tuendelee kutoa ushirikiano kwa viongozi wetu hususan kwa askari Polisi, wapo kituoni hapa kuna jambo lolote unalolihisi hawa ndio usalama wako usisite fika, kuna ushahidi wako unahitajika njoo toa, ndio tunajenga Tanzania hii yenye Amani” amesema Ndugu Geraruma.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa amewataka viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kufikiria kujenga nyumba za Askari polisi karibu na kituo hicho cha Polisi hao ili kurahisisha utendaji kazi wa askari polisi hao lakini pia kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi.
Amesema sio sahihi na haipendezi kabisa kukimbia au kutotoa ushahidi pale ambapo unapohitajika ikiwa ni pamoja na ushahidi unaohusu masuala ya ubakaji ili wale wanaotuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa amewataka askari polisi kutenda haki pale wanapopelekewa mashauri mbalimbali ya uvunjaji wa sheria, amesema wanatakiwa kuchukuliwa hatua wachukuliwe na asiyehusika aachiliwe huru aendelee na kazi ya kuijenga nchi yake.
Mwenge wa Uhuru kesho unatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ikiwa ni Halmmashauri ya saba kati ya Halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.