Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Luteni Josephine Paul Mwambashi amewataka wananchi wa Kijiji cha Miwangani Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro kutunza vyanzo vya maji ili kuondokana na kero ya maji waliyokuwa wakiipata hapo awali.
Luteni Josephine Mwambashi ametoa wito huo Agosti 7 mwaka huu wakati akizindua mradi wa maji uliopitiwa na Mwenge wa uhuru kukagua na kuridhishwa utekelezaji wake wenye lengo la kuboresha miundo mbinu ya mradi huo wa maji mserereko ambao ulisimamiwa na RUWASA wakishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero (Mlimba) pamoja na wananchi.
Aidha, Kiongozi huyo wa mbio za mwenge amebainisha faida za kutunza chanzo vyanzo vya maji pamoja na miundombin yake hususan katika kijiji hicho kuwa ni kutosababisha maji ya mradi huo kukauka na hivyo kuwaondolea adha wananchi kufuata maji umbali mrefu zaidi.
Amesema, hapo awali akina mama na watoto walitumia muda mrefu kufuata maji mbali na kusababisha shughuli nyingine kusimama huku wanafunzi nao kutumwa kutafuta maji na kuacha masomo jambo ambalo liliwacheleweshea maendeleo yao.
“tunaendelea kusisitiza wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa sababu mradi huu unatunufaisha sana kama tulivyosomewa kwenye taarifa, lakini uwepo wa mradi huu umesaidia sana akina mama na watoto kutumia muda waliokuwa wanafuata maji mbali kufanya shughuli nyingine…” amesema Luteni Josephine.
Kwa sababu hiyo amewataka wananchi wa Kijiji cha Miwangani kutunza chanzo cha maji cha mradi huo pamoja na miundombinu yake ili muda ule waliokuwa wanautumia awali kwenda umbali mrefu kutafuta maji sasa wautumie katika kujiletea maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi pamoja na Kuishukuru Serikali ya awmu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Kutoa fedha kwa ajili ya Mradi huo, ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Kijiji cha miwangani kwa kuunganisha nguvu zao na kuwezesha kuchimba mtalo wa kulaza mabomba umbali wa zaidi ya Km.6.4.
Awali Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilombero Frolence Mlelwa akisoma taarifa ya Mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio maaluma za Mwenge wa Uhuru amesema mradi huo ambao utatoa manufaa kwa wakazi wa Miwangani zaidi ya 2004 hadi kukamilika kwake umegharimu fedha za kitanzania 130,176,878.00.
Aidha, amesema kati ya kiasi hicho cha fedha, Tsh. 27,613,000.00 ni nguvu za wananchi zimetumika kupitia kuchimba mfereji kwa ajili ya kulaza mabomba ya maji ya mradi huo.
Mwenge maalumu wa Uhuru unaendelea na mbio zake Mkoani Morogoro ikiwa ni siku yake ya Nne tangu uanze kukimbizwa Mkoani humo na leo uko Wilayani Kilombero ambapo umepitia miradi ya maendeleo saba ukiwemo mradi huo wa maji mserereko ambao umezinduliwa leo, Agosti 8 Mwenge wa uhuru utakimbizwa katika Wilaya ya Mvomero.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.