KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA ATOA WIKI MOJA KUPATA HATI YA KIWANJA CHA MRADI
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfley Mnzava ametoa wiki moja kwa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kutafuta hati miliki ya kiwanja cha mradi wa upanuzi wa maji uliopo Kijiji cha Makuyu ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati mradi huo umeanza kutoa matunda na kunufaisha wananchi kama ulivokusudiwa wa kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi wa vijiji lengwa
Kiongozi huyo wa Mbio Mwenge Kitaifa ametoa agizo hilo leo Aprili 21 wakati akizindua mradi wa upanuzi wa miundombinu ya maji katika Kijiji cha Makuyu unaolenga kuwanufaisha wananchi wa vijiji vya Kinyolisi na Iyogwe.
Aidha, ameagiza Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA Pamoja na kuwa eneo hilo limetolewa na wananchi ili wapate maji bado wanatakiwa kufuatilia makubaliano hayo kuwekwa kimaandishi ili nyaraka hizo ziweze kusaidia mchakato mzima wa kuipata hati hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Gairo Mhandisi Gilbert Isac amesema mradi huo unakwenda sambamba na kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani huku akibainisha kuwa mradi huo unakwenda kunufaisha wananchi zaidi ya 6,000 hivyo kupunguza umbali mrefu waliokuwa wanaupata wananchi hao wa kutafuta maji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Iyogwe ambaye ni mmoja wa Vijiji nufaika Bw. Richard Yeremia Kagoda, amesema kutokana na changamoto ya maji waliokuwa wanaipata siku za nyuma na baada ya kuona Serikali imekuja na mradi huo, waliamua kutoa eneo hilo bure kwa Serikali ili mradi huo uweze kutekelezwa haraka.
Mradi huo unaogharimu Tsh. 513,050,359.33 bila VAT umelenga kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa jamii ambao Fedha zake zimetolewa na serikali Kuu kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.