Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI anayeshughulikia Afya Bi. Grace Magembe amemuagiza kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Ndelisho Moshi pamoja na Mganga Mfawidhi wa Halmashauri hiyo kuwa hadi kufikia Jumatatu ya wiki ijayo kituo cha Afya cha Mikese kianze kutoa huduma ya Afya Kwa wananchi wa Tarafa hiyo kutokana na kukamilika kwa miundombinu yote muhimu.
Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa agizo hilo Februari 6 mwaka huu kwenye ziara yake iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya na kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya.
Aidha, Bi. Grace amesema ameridhishwa na ujenzi wa kituo hicho ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 100 suala lililobakia ni utoaji wa huduma Kwa wananchi na kuagiza kuwa Halmashauri ishughulikie suala la vifaa tiba pamoja na dawa ili wananchi wapate huduma mara moja.
“...Jumatatu huduma zianze kutolewa kwenye jengo hili...” ameagiza Bi. Grace Magembe.
Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa Serikali imetoa fedha kiasi cha Shilingi million 400 Kwa ajili ya ujenzi wa majengo matano yakiwemo jengo la huduma ya mama na mtoto, Maabara, Wodi ya wazazi na jengo la dharura.
Sambamba na hilo, Naibu Katibu Mkuu huyo akiwa katika Zahanati ya Kijiji cha Fulwe amewahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa ili waweze kupunguza gharama za matibabu ambazo wanakutana nazo.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Mikese Mhe. Saidi Kimbeho ameeleza changamoto ya baadhi ya majengo na vifaa kuto tumika katika Zahanati ya Kijiji cha Fulwe na baadhi ya madaktari kuhamishwa hivyo kufanya baadhi ya huduma muhimu kama za maabara kukosekana.
Sambamba na changamoto hiyo bado amesema gari la kubebea wagonjwa ni moja kwa Halmashauri nzima hivyo inaleta changamoto kwa wagonjwa wanaopata rufaa kwenda hospitali ya Mkoa kwa matibabu zaidi.
Nae Bi. Godliver Majige Mkazi wa Kata hiyo ya qMikese ameishukuru na kuipongeza Serikali pamoja na wahudumu wa Zahanati ya Fulwe kwa kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa wananchi hao ni za uhakika na kutoa ombi kwa Naibu Katibu Mkuu huyo kuboresha huduma nyingine zikiwemo za maabara pamoja na kuongeza wahudumu wake ili kuleta ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma hizo za afya.
Ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu huyo ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo alilolitoa wakati wa ziara yake hivi karibu katika Wilaya hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa na wananchi wananufaika mataibabu yanayotolewa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.