Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewapongeza wawekezaji wa kiwanda cha sukari cha Kilombero ambacho kinazalisha asilimia 26 ya sukari inayotumiwa hapa nchini, na kuwataka kuweka mazingira mazuri kwa wakulima ili uzalishaji huo uongezeke.
Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero.
Waziri Kijaji ametoa pongezi hizo Agosti 10 mwaka huu alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kukagua hali ya uzalishaji wa sukari na maendeleo ya ujenzi wa kiwanda kipya cha sukari kinachoongezwa ikiwa ni ziara yake ya siku mbili Mkoani Morogoro.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wakipanga pakti za sukari iliyokuwa tayari ili kupelekwa sokoni.
Waziri huyo amesema nchi ina viwanda vikubwa zaidi ya vitano ambavyo vinazalisha sukari kikiwemo kiwanda cha sukari cha Kilombero, Mtibwa, Kagera, TPC - Moshi na Bagamoyo lakini asilimia 26 ya sukari inazalishwa na kiwanda cha sukari cha Kilombero, hivyo ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa uwekezaji wao na kazi nzuri wanayoifanya.
“…niwapongeze wawekezaji wa Kilombero sugar kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika…wao ni wazalishaji wa asilimia 26 ya sukari yote tunayotumia ndani ya nchi yetu…” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Waziri huyo amepongeza kazi kubwa ya ujenzi wa Kiwanda unaoendelea kwa ajiri kuongeza ukubwa wa kiwanda hicho ambacho ujenzi wake unagharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 500 na kwamba hiyo itasaidia wakulima wa miwa katika maeneo hayo hawatapata changamoto ya soko la miwa yao.
Katika hatua nyingine Waziri Kijaji amesema mwaka 2019 Serikali ilianzisha Mpango wa kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji Biashara nchini (MKUMBI) mpango ambao umefanikiwa kwa asilimia 80 ambapo wawekezaji wengi wamefika nchini kuwekeza katika maeneo tofauti tofauti.
Aidha, Dkt. Kijaji amebainisha kuwa Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya kodi ya mwaka 2023 ambayo imeanza kutumika tangu Julai 2023 kwa kuondoa na kufuta tozo na kodi ambazo zilikuwa ni miongoni mwa kikwazo cha wawekezaji na wafanyabiashara hapa nchini lengo ni kuvutia wawekezaji.
Waziri wa Biashara na Viwanda Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amepongeza mikakati iliyowekwa na uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwapatia elimu wakulima kupitia maafisa ugani ambao wanachochea uzalishaji wa miwa wenye tija.
Aidha, amesema usajili wa wakulima kielektroniki unasaidia kuwatambua na kuwafikia wakulima katika maeneo waliyopo.
Waziri Kijaji, RC Malima, DC Kyobya, uongozi na wataalamu mbalimbali wa kiwanda cha sukari cha Kilombero wakitembelea kiwanda hicho.
Naye, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Guy William amemshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara ambapo amebainisha kuwa utanuzi wa kiwanda hicho utazalisha tani 271,000 za sukari na uzalisha huo utaondoa upungufu wa sukari nchini.
Mkurugenzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero Bw. Guy William akibainisha namna ya utendaji kazi baada ya kukamilisha upanuzi wa kiwanda hicho.
Hadi sasa ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 60 na kinatarajia kuanza uzalishaji wake ifikapo Julai 2024.
Ziara ya Waziri Kijaji itaendelea Agosti 11, 2023 kwa kutembelea kiwanda cha Mkulazi kilichopo Mbigiri Wilayani Kilosa kuona maendeleo ya ujenzi huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.