Kiwanda cha Sukari cha Kilombero cha Mkoani Morogoro kinatazamiwa kuzalisha sukari tani 270,000 kwa mwaka mara kitakapokamilika ujenzi wake huku Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima akiridhishwa na ujenzi wa Kiwanda hicho kipya cha K4 unaoendelea.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anaangalia uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha sasa kinachofanya kazi.
Hayo yamefahamika wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro alipofanya ziara Julai 22 mwaka huu kwa lengo la kujionea upanuzi wa Kiwanda hicho huku akionesha kuridhihwa na hatua iliyofikiwa.
Hili ni eneo ambalo kiwanda kipya cha sukari cha 4k kinajengwa.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa ameweka bayana kuwa kiwanda hicho cha kisasa kinachojulikana kama K4 kitakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 270,000 za sukari kwa mwaka.
Meneja wa kiwanda cha sukari cha kilombero Be. Guy William (wa tatu kushoto) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Adam Malima (wa pili kulia) wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kiobya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama.
"...kiwanda cha hapa Kilombero kitakuwa na uzalishaji wa tani 270,000, kile kiwanda cha miaka ya 60 cha zamani kinafungwa kwa hiyo tumepata bahati ya kwenda kukiona kinafanya kazi vizuri ila kinatumia nishati na gharama kubwa za uendeshaji" amesema Mhe. Malima.
Aidha, ameongeza kuwa kiwanda cha sasa kinatumia teknolojia ya miaka 60 iliyopita hivyo hutumia nishati na gharama kubwa kwa sababu hiyo kinapelekea kupanda kwa bei ya sukari, hata hivyo amebainisha kuwa kiwanda kinachojengwa sasa kitaleta ajira zaidi na unafuu kwa gharama ya sukari na gharama za uendeshaji wa Maisha kwa wananchi.
Mhe. Malima ameendelea kusema wawekezaji wa kiwanda hicho wanapaswa kuweka mikakati na kutoa elimu kwa wakulima kwenda sambamba na kasi ya uzalishaji wa kiwanda hicho cha kisasa ili wakulima hao wawe na uhakika na kulima mashamba makubwa huku kukiwa na uhakika wa masoko ya miwa inayolimwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima ameipongeza serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na amani ambayo inayochochea uwekezaji mkubwa ukiwemo wa kiwanda hicho cha Sukari cha Kilombero huku akiwahakikishia wawekezaji wa kiwanda hicho usalama wa uwekezaji wao.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakiangalia ujenzi wa kiwanda kipya cha sukari ambacho ujenzi wake unaendelea.
Lakini pia Mhe. Adam Malima amempongeza Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (Kilombero sugar Company Limited) Guy William kwa kuonesha ushirikiano kwa Serikali hususan Katika kuchangia mapato ya nchi kwa kulipa ushuru unaostahiri kupitia Halmashauri za Ifakara Mji na Kilosa.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero Bw. Fimbo Butara amesema bidhaa za sukari zina ubora ambao kila mwananchi anaweza kutumia kulingana na kipato chake kwani vipo vifungashio vya sukari hadi vya shilingi 200 hivyo amewataka wananchi kuendelea kutumia Sukari inayozalishwa Kiwandani hapo kwa sababu ina gharama nafuu na ina ubora unaohitajika.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima akiangalia mchakato wa uzalishaji sukari katika kiwanda cha sukari kilombero.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari Bw. Filbert Mpozi amesema hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania haitaagiza sukari kutoka nchi za nje kutokana na kuwa na sukari ya kutosha hapa nchini hivyo amewapongeza wawekezaji wa kampuni hiyo ya uzalishaji Sukari ya Kilombero.
Asilimia 75 ya kiwanda cha Sukari cha Kilombero kinamilikiwa na Illovo huku asilimia 25 ni Umiliki wa Serikali ya Tanzania na kina mchango mkubwa kwa jamii inayokizunguka kwa kutoa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.
Kiwanda hicho hadi kukamilika kwake mwezi Julai mwakani kitagharimu Bil. 600 na kitazalisha tani 270,000 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo kinazalisha tani 130,000 pekee kwa mwaka.
Moja ya mtambo unaotumika kubeba miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari kiwandani.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.