Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekipongeza kiwanda kipya cha Sukari cha Mkulazi kwa mikakati iliyowekwa na wawekezaji wa kiwanda hicho ya kuzalisha tani zaidi ya 20,000 za sukari na kuondoa utegemezi wa kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.
Waziri Kijaji amebainisha hayo Agosti 11 mwaka huu alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mbigiri Wilayani Kilosa na kujionea maendeleo na hatua za ujenzi wake.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka katika kiwanda cha sukari Mkulazi.
Waziri huyo amesema Serikali huagiza tani 250,000 za sukari ya viwandani kwa mwaka hivyo, kiwanda hicho licha ya kuzalisha sukari ya matumizi ya majumbani lakini pia itazalisha sukari ili kulisha viwanda vinavyotumia mali ghafi hiyo.
“...kitu cha kupongeza katika kiwanda hiki ni kwamba kati ya viwanda vitano vikubwa tulivyonavyo hapa nchini hakuna hata kiwanda kimoja kinachozalisha sukari ya viwandani hivyo tunalazimika kuagiza sukari yote ya viwandani kutoka nje ya nchi...” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imejenga kiwanda hicho na kufunga mifumo ya kuzalisha sukari hiyo ili ifikapo mwaka 2030 Serikali isiagize sukari kutoka nje.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji hususan Mkoani humo.
Aidha, amesema kiwanda cha sukari cha Mkulazi ni cha kimkakati kwa kuwa kitasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kuagizia sukari nje ya nchi na kwamba kiwanda hicho kipya ni mfano kwa viwanda vingine.
Baadhi ya mitambo ya kuzalisha sukari katika kiwanda kipya cha sukari Mkulazi.
Naye, Mkurugenzi wa Udhibiti kutoka Bodi ya Sukari Bw. Lusomyo Buzingo amesema uzalishaji wa sukari unaotarajiwa kufanyika kiwandani hapo ni takribani tani 50,000 hadi tani 75,000 kwa mwaka utaongeza uzalishaji wa sukari kufikia tani 490,000 hivyo kupunguza uagizaji wa sukari kutoka nje na kupunguza matumizi ya pesa za kigeni.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiwa na Mhe. Adam Malima pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Mkulazi katika kikao kifupi cha kupokea taarifa ya kiwanda hicho.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.