Kiwanda cha Tumbaku Morogoro chaanza kazi, wakaulima wahamasishwa kulima zao hilo.
Kiwanda cha kuchakata zao la Tumbaku cha Mkoani Morogoro kilichojulikana kwa jina la TLTC kimeanza kazi ya kuchakata zao hilo baada ya kusimama kwa takribani miaka minne iliyopita.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kulia) akipata maelezo ya mashine za tumbaku kutoka kwa mwekezaji wa kiwanda hicho Bw. Ahmad Huwel wakati ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa alipotembea kiwanda hicho Juni 10 Mwaka huu.
Taarifa hiyo njema kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro na watanzania kwa ujumla imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela Juni 10 mwaka huu alipokitembelea kiwanda hicho ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Kata zote za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro aliyoianza mwanzoni mwa wiki hii kwa ajili ya kutembelea miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Baada ya kutembelea na kuongea na uongozi wa kiwanda hicho cha tumbaku Martine Shigela amesema kiwanda hicho kilikuwa kimeajiri watu zaidi ya 3000 na wote walipoteza kazi baada ya kiwanda hicho kusimama, hata hivyo amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ushawishi wake na kuona shehena ya zao hilo kutoka mikoani kuanza kuingia na baadhi ya wafanyakazi kiwandani hapo wakiwa kazini.
Aidha, amepongeza jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua nchi na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini na kumpongeza mwekezaji mzawa wa kiwanda hicho kwa kushawishika kuja kuendesha kiwanda hicho.
Shigela ametoa wito kwa wakulima wa zao la tumbaku kuanza kulima kwa wingi zao hilo kwa kuwa sasa wana uhakika wa kupeleka tumbaku yao katika kiwanda hicho ambacho kimeanza kufanya kazi.
“kwa hiyo kuna gap la tani elfu sabini ambazo kama wakulima na wananchi tuhamasike kwenda kuzalisha tumbaku kwa wingi kwa sababu tuna uhakika wa soko” amesema Martine Shigela.
Kwa upande wake Mwekezaji mzawa wa kiwanda hicho kutoka Mkoani Iringa Bw. Ahmed Huwel ameishukuru Serikali kwa kuonesha ushirikiano na kumshawishi kuwekeza katika sekta na kutamka rasmi kuwa kiwanda sasa kimerudi nyumbani hivyo amewaomba wananchi kulima tumbaku kwa wingi na kwamba malengo yake kufikisha tani 120,000 ifikapo mwaka 2025 hivyo kutoa ajira ya kutosha kwa wananchi.
Mwekezaji mpya wa kiwanda cha tumbaku Bw. Ahmad Huwel akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela juu ya tumbuku inavyochakatwa kiwandani hapo wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa Juni 10 mwaka huu.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Hussein Bashe kuwa Waziri wa Kilimo kwa kuwa amesema ni kiongozi mahili kiutendaji na mfuatiliaji wa mambo.
Aidha, amemshukuru Waziri Bashe kwa jitihada zake ambazo alianza kuzifanya tangua akiwa Naibu Waziri katika Serikali ya awamu ya tano kwa kuhangaika kukirudisha kiwanda hicho hadi jitihada zake kuzaa matunda akiwa Waziri katika ya Serikali ya awamu ya sita, na kwamba jitihada zake zinakwenda kuwakomboa kiuchumi wananchi zaidi ya 5,000 pamoja na familia zao waliaokuwa wameachishwa kazi wakati kiwanda hicho kimesimama.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando ambaye kiwanda hicho kipo katika eneo lake ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa uongozi wa kiwanda hicho na kwamba hayuko tayari kuona kiwanda hicho kinasimama tena kwa changamoto zozote ambazo zitakuwa ndani ya uwezo wake.
Imeelezwa kuwa kiwanda hicho cha tumbaku kina uwezo wa kuchakata tani 120,000 kwa mwaka ambapo sasa kinachakata tani elfu 50 tu kwa sababu ya kukosa mali ghafi hivyo kuwa na upungufu wa tani elfu 70 na kwamba uhamasishaji wa dhati wa kilimo cha tumbaku unahitajika hususan mikoa inayolima zao hilo ili kuendesha kiwanda hicho.
Baadhi ya shehena ya mizigo ya zao la tumbaku ikionekana katika kiwanda hicho kilichopo Mkoani Morogoro tayari kwa kuanza kazi ya uzalishaji.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.