Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema mikoa minne inayounda Nanenane kanda ya mashariki ina mkakati wa kuhakikisha ifikapo 2024 mazao ya korosho na pamba yazalishwe kuanzia tani 20,000 hadi 30,000 ili kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa nchi.
Adam Malima amesema hayo Agosti 5, 2023 alipotembelea vipando vya Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo vilivyopo katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yanayoendelea kufanyika mara baada ya kufunguliwa na Waziri Msaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mizengo Pinda hapo Agosti Mosi mwaka huu.
"... Kanda ya Mashariki ndio Kanda kubwa, hivyo tumepeana mikakati ya makusudi kwamba mwakani tunaanza kuhakikisha Kanda hii inachangia kwenye uzalishaji wa Taifa kuanzia tani 20000 hadi 30000 za korosho..." amesema Mhe. Adam Malima
Amesema, serikali inampango mkakati huo ili kuwa na mazao mbadala, huku akitolea mfano wa mazao mbadala hayo kuwa ni pamoja na Karafuu na hiriki, hivyo amewataka wakulima kujifunza kilimo cha korosho kwa umakini mkubwa katika maonesho hayo.
Aidha, Mhe. Malima amesema katika kikao cha tathmini cha viongozi wa Kanda ya Mashariki kitajikita kuweka mikakati ya uzalishaji wenye tija wa mazao mbadala ili kushika namba moja kitaifa kwa uzalishaji wa mazao hayo.
Sambamba na hilo, Mhe. Malima amesema wananchi wanatakiwa kuondoa dhana ya kilimo kuwa ni cha watu wa hali ya chini bali kilimo ni kazi inayohitaji mtaji kidogo faida kubwa, hivyo amewataka wananchi kujitokeza katika maonesho hayo kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kwa uzalishaji wenye tija Zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Kanali Maulid Hassan Surumbu akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amesema amefurahishwa na Maonesho hayo huku akiweka bayana kuwa Wilaya yake ina shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo uvuvi, Kilimo cha zao la Mwani, uchimbaji wa madini aina ya jiwe la Tanga (Tanga stone) ambalo hutumika kujengea nyumba, huku akiwataka wakulima kutembelea vipando vya Halmashauri ya wilaya ya Mkinga kupata elimu zaidi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.