Lishe bora na huduma zingine za msingi kama elimu na afya ni haki ya kila mtoto kwa mujibu wa Mhe. Fatma Mwassa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro lakini mara nyingi watoto hukosa lishe bora kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo hali ya kipato, kutokuwa na elimu sahihi kuhusu Lishe bora pamoja na mila na desturi za jamii.
Amesema hayo agosti 8, 2022 katika kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
"udumavu huu wa akili hupelekea mamilioni ya watoto kuwa na tatizo la akili na kusababisha tatizo kwa jamii nzima... tunatakiwa kutoa elimu ya Lishe bora, kwani ni haki ya Msingi kwa kila mtoto kwa maendeleo ya jamii..." amesema Mhe. Fatma Mwassa
Mhe. Mwassa amesema hali hiyo inaweka afya za watoto hatarini kwani hupelekea tatizo la udumavu wa akili na kujenga jamii yenye tatizo la Afya ya akili, na utapiamlo kwa kukosa lishe bora, lakini wengine hata hushindwa kuhudhuria masomo katika shule zao.
Nae Bi. Salome Magembe, Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro amesema kuna idadi kubwa ya watoto wenye udumavu ambapo utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionesha 26.4% sawa na watoto 100,730 wana udumavu kwani hali hiyo hupunguza nguvu kazi kimwili na kiakili na kuchochea changamoto za uzalishaji katika Taifa.
Sambamba na hilo, Bi. Salome amesema mikakati iliyowekwa katika kikao hicho ni kutoa elimu ya lishe kwa jamii kupitia viongozi mbalimbali wakiwemo maafisa watendaji wa Kata na maafisa Lishe waliopo katika Halmashauri zote 9 za Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake, Bw. Simon Mkali Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mlimba, Mkoani Morogoro amesema mila na desturi ni changamoto kubwa kwa jamii hizo kwani wazazi hushindwa kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo, sambamba na hilo amesema kuwa wanajukumu kubwa la kuelimisha jamii ili kujenga jamii yenye uelewa kuhusu Lishe bora.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.