Kuna swali linaulizwa na baadhi ya watanzania, lishe bora ni nini?
Lishe bora maana yake ni kula chakula cha kutosha na chakula kinachofaa ili kusaidia mwili kukua vyema, kuwa na afya na uwezo wa kupigana na magonjwa mbalimbali.
Lakini pia maswali mengi yanaulizwa, ni nini umuhim wa lishe?
Lishe bora inaumuhim katika mwili wa mwanadamu ni pamoja na kuupa mwili nguvu ya kupambana na magonjwa, kuharakisha ukuaji wa mtoto na mwili kuwa na kinga.
Ni nini haswa madhara ya kukosa lishe bora?
Madhara ya ukosefu wa lishe bora ni pamoja na mtoto kudumaa, Ngozi yake kusinyaa, kukumbwa na utapiamlopamoja na kwashakoo.
Katika maeneo mengi nchini Tanzania watu wengi wao hula chakula aina moja ambacho hakina gharama ya juu kwa kila mlo yaweza kuwa wali, mahindi, viazi, au ndizi.
Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo imekuwa haifanyi vizuri katika suala la lishe.
Kufuatia hali hiyo, Wizara ya Afya iliandaa maadhimisho ya siku ya lishe ambayo kitaifa ilifanyika Oktoba 29,2022 katika viwanja vya Fulwe, Tarafa ya Mikese Wilaya ya Morogoro na mgeni rasmi alikuwa Dkt. Godwin Mollel Naibu Waziri wa Afya.
Lengo la maadhimisho hayo yalilenga kuwakutanisha wadau wa afya na lishe ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa lishe bora.
Akitoa tathmini ya lishe katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ameeleza kuwa hali ya udumavu kwa Watoto chini ya miaka miwili ni asilimia 26.4, na upungufu wa damu kwa watu kati ya umri wa miaka 15 na 49 ni asilimia 29.8 hivyo kufanya Mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa ambayo haijafanya vizuri katika suala la lishe.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akitoa tathmini ya lishe ya katika Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Mkoa huo unashika nafasi ya nne katika uzalishaji wa chakula hapa nchini, lakini umekuwa ndio miongoni mwa mikoa ambayo haifanyi vizuri kwenye lishe, na sababu kubwa ni wananchi kutokuwa na elimu ya matumizi ya chakula kwa ajili ya lishe.
Sambamba na hilo Mhe. Fatma Mwassa amewataka wadau wa lishe kujikita katika kutoa elimu ya lishe mashuleni na kupitia mitandao ya kijamii kama ‘Online tv’.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka viongozi wa dini katika Mkoa huo kuwaelimisha waumini wao kuhusu matumizi ya lishe bora.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akizungumza na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa.
Aidha, Dkt. Mollel amewaagiza wadau wa lishe kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, TAMISEMI, na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuangalia namna ya kupata mashine zitakazotumika kuongeza virutubishi vya lishe kwenye chakula.
Amesema, mashine hizo zikipatikana wapewe vijana ili wajikwamue kiuchumi na katika kufanya hivyo tatizo la lishe duni katika Mkoa huu na Taifa kwa ujumla litapungua kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hilo amewataka wazazi kuchangia chakula cha watoto wao mashuleni ili kupunguza changamoto ya utoro kwa wanafunzi wakati wa masomo.
Nao watoa huduma za afya walipata nafasi ya kutoa ujumbe kwa jamii juu ya uzingatiaji wa lishe kwa mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano kuzingatia ulaji wa makundi matano ya vyakula.
Watoa huduma hao walibainisha makundi hayo matano ya vyakula ni pamoja na matunda, vyakula jamii ya kunde, mboga mboga, jamii ya mizizi na vyakula vya mafuta kama karanga.
Mfano wa makundi ya vyakula vinavyotakiwa kuliwa na wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na watu wa lika zote.
Kula vyakula vyote kutoka kwenye makundi hayo matano ndiko tunaita Lishe Bora na jamii yote ikifanikiwa kupata vyakula hivyo itakuwa na Afya inayowawezesha kujishughulisha uzalishaji mali, kukuza uchumi kwa kwani LISHE BORA NI MSINGI WA MAENDELEO.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.